ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Wednesday, September 12, 2018

DIWANI AZOMEWA MBELE YA MKUU WA WILAYA.





Na Ahmed Mmow, Kilwa
DIWANI wa kata ya Njinjo wilaya ya Kilwa, Ashura Kuchao amejikuta katika wakati mgumu kufuatia kuzomewa na wananchi mbele ya Mkuu wa Wilaya hiyo Christopher Ngubiagai.

Zomeazomea hiyo ilitokea  katika mkutano wa hadhara ulioitishwa na Mkuu huyo wa wilaya ili kusikiliza kero za wananchi hao.

Ngubiagai alikwenda kijijini hapo kufuatia wananchi hao kumlalamikia mwenyekiti wao wa kijiji Abdulmalick Mnakatu kushindwa kuitisha mikutano mikuu ya kijiji tangu alipochaguliwa na wananchi.

Mwenyekiti ambaye alitangaza kujiuzulu siku moja baada ya kusikia ziara ya Mkuu wa Wilaya alipata fursa ya kusalimiana na Mkuu huyo wa wilaya na kumweleza kuwa mikutano ilikuwa haifanyiki kwa sababu wajumbe wake wengi wa Halmashauri ya kijiji walikuwa bize na kilimo hivyo alishindwa kuwapata kila alipokuwa akiwahitaji.

Wakati wa mkutano huo, Mkuu wa wilaya alianza kupokea kero za wananchi ambapo wananchi mbalimbali walieleza kuwa diwani wao hajaitisha mikutano na wananchi kutoa taarifa za mapato na matumizi na fedha zinazoletwa na serikali ngazi ya kata na kibaya zaidi hata kero za wananchi hazijui.

“Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya, sisi tunavyofahamu diwani anatakiwa akusanye kero kutoka kwetu lakini diwani wetu hajawahi kukutana na sisi hata siku moja na kila siku anakwenda kwenye vikao vya Halmashauri, hizo kero anazopeleka huko anazitoa wapi.” Alisema mwananchi mmoja na kusababisha wananchi wapige makofi.

Kutokana na kero hiyo, Mkuu wa Wilaya aliwaambia wananchi hao kuwa kero hiyo anatakiwa aijibu diwani mwenyewe ambapo alipompa nafasi hiyo, diwani huyo aliwaambia wananchi kuwa yeye anasikiliza kero kutoka kwa watendaji wa vijiji na anazipeleka Halmashauri.

“Mimi nasubiri kero kutoka kwa watendaji wa vijiji na ndio nazipeleka Halmashauri, habari ndio hiyo” alisema diwani huyo na kusababisha hasira kwa wananchi hao.

Wananchi hao waliendelea kumuuliza Mkuu wa Wilaya diwani huyo anazipata wapo kero za wananchi hao wakati vijiji vyenyewe havifanyi mikutano na ndio sababu ya kumuomba Mkuu wa Wilaya afike kijijini, hata hivyo diwani huyo aligoma kujibu swali hilo akidai ameshawazoea wananchi hao, hivyo hawamsumbui.

Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya aliwaambia wananchi hao kuwa akili ziko kichwani mwao na kwamba uchaguzi unakuja, hivyo adhabu ya viongozi wa kuchaguliwa iko mikononi mwao.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.