Saturday, April 9, 2022
ULEGA-TUTAENDELEA KULINDA RASILIMALI ZA UVUVI ILI ZIWALINDE WATANZANIA
WAAMUZI 6, KUCHEZESHA SIMBA Vs ORLANDO
Katika mchezo huo itatumika teknolojia ya usaidizi kwa njia ya televisheni kwa waamuzi VAR. na kwa mujibu wa CAF michezo yote ya hatua ya robo fainali teknolojia hii itatumika. Lakini itakuwa ni kwa mara ya kwanza VAR inatumika nchini Tanzania.
Waamuzi watakaochezesha mchezo huo, Mwamuzi wa kati ni Haythem Guirat kutoka Tunisia, Mwamuzi msaidizi namba 1 (Line 1) ni Khalil Hassan wa Tunisia, msaidizi namba 2, (Line 2) ni Samuel Pwadutakam kutoka Nigeria na mwamuzi wa mezani yani Fourth official ni Sadom Selmi wa Morocco
Na waamuzi watakaosimamia VAR ni Ahmed Elghandour wa Misri na msaidizi ni Youssef Wahid.
Lakini pia katika mchezo huo klabu ya Simba imeruhusiwa kuingiza mashabiki Elfu 60 (60,000) uwanjani katika mchezo huu, ikiwa ni kwa mara ya kwanza msimu huu. Katika michezo iliyopita walikwa wakiruhusiwa kuingiza mashabiki Elfu 35 (35,000) ambao ulikuwa ni mpango wa kujinginga na maambukizi ya Uviko 19.
WILL SMITH APIGWA MARUFUKU KUSHIRIKI OSCAR KWA MIAKA 10.
Will Smith amepigwa marufuku kushiriki katika Oscars and matukio mengine ya Academy kwa miaka 10 baada ya kumchapa kibao muigizaji na mchekeshaji Chris Rock wakati wa hafla ya Oscars.
Academy of Motion Picture Arts and Science ambayo huandaa sherehe za kutoa tuzo, ilikuwa kwa njia ya mtanda Ijumaa kujadili hatua za kinidhamu. Smith aliomba msamaha kwa vitendo vyake na kujiuzulu kutoka Academy.
Smith alimchapa kibao Rock kwa kumfanyia utani mke wake ambaye alikuwa amekata nywele, ikiwa ni kutokana na hali ya kiafya ya ugonjwa unaojulikana kama alopecia ambao humfanya mtu kunyonyoka nywele.
Chini ya saa moja baadaye, alipewa tuzo ya muigizaji bora kwa uigizaji wakati kama “King Richard,” ambapo aliigiza kama baba wa nyota wawili wa tennis Venus na Serena Williams.
Katika taarifa yake, Academy ilisema kuwa Oscars “iligubikwa na tabia mbaya na isiyokubalika hata kidogo ambayo Bwana Smith aliionyesha jukwaani.”
WAVUVI WATAKIWA KUACHA KUFANYA KAZI KWA MAZOEA KUEPUKA VIFO, KUPOTEZA MALI
AFISA Mfawidhi wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) Mkoani Tanga Captain Christopher Shalua kulia akiwaonyesha wavuvi wa namna ya kuvaa vifaa vya kujiokolea wanapokuwa majini wakati alipokwenda akizungumza na wavuvi, wamiliki wa vyombo, manahodha na wananchi wa Vijiji vya Monga Vyeru wilayani Mkinga mkoani Tanga kutoa elimu ya umuhimu wa usalama na utunzaji wa mazingiraAFISA Mfawidhi wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) Mkoani Tanga Captain Christopher Shalua kulia akisisitiza jambo wakati akizungumza na wavuvi, wamiliki wa vyombo, manahodha na wananchi wa Vijiji vya Monga Vyeru wilayani MkingaAFISA Mfawidhi wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) Mkoani Tanga Captain Christopher Shalua kulia akizungumza jambo wakati akizungumza na wavuvi, wamiliki wa vyombo, manahodha na wananchi wa Vijiji vya Monga Vyeru wilayani Mkinga
Afisa Mfawidhi wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) Mkoani Tanga Captain Christopher Shalua kulia akifuatilia kwa umakini maswali kutoka kwa wavuvi,wamiliki wa vyombo |
Afisa Masoko Mwandamizi wa Shirika la TASAC Martha Kalvin akieleza jambo kwa wavuvi kuhusu umuhimu wa usalama wawapo kwenye shughuli zao |
NA OSCAR ASSENGA, TANGA.
SHIRIKA la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limesisitiza umuhimu wa wavuvi kuzingatia usalama ikiwemo kuwataka kuacha kufanya kazi kwa mazoea wanapokuwa katika shughuli za Uvuvi wawapo majini ili kuwaepusha na vifo,majeruhi na kupoteza mali.
Huku wakisisitiziwa umuhimu wa kuwa na vifaa vya kujiokolea wanapokuwa majini ili viweze kuwasaidia kuepukana na ajali ambazo wanaweza kukumbana nazo.
Wito huo ulitolewa leo na Afisa Mfawidhi wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) Mkoani Tanga Captain Christopher Shalua wakati na akizungumza na wavuvi, wamiliki wa vyombo, manahodha na wananchi wa Vijiji vya Monga Vyeru wilayani Mkinga na Mwalo wa Sahare Jijini Tanga mkoani Tanga walipokwenda kutoa elimu ya umuhimu wa usalama na utunzaji wa mazingira.
Alisema kwamba ni muhimu kwao kuweza kuhakikisha wanazingatia usalama wakati wanapokwenda kufanya shughuli zao kwani hilo litawaepusha na majanga ambayo wanaweza kukutana nayo na kupelekea kupata majeraha au kupoteza maisha na mali.
“Serikali imeona hilo ni jambo la msingi sana na ndio maana tumeona leo tuje hapa Monga Vyeru kuwapa elimu hii ya usalama na utunzaji wa mazingira hususani mnapokuwa kwenye shughuli zenu hili ni jambo hilo lakini pia kuhakikisha mnakuwa na vifaa vya uokozi”Alisema
“Kwani tunatambua kwamba pia wavuvi wana familia hivyo elimu hii itaweza kuwasaidia kupunguza ajali,kuondoa vifo na kupunguza majeruhi na kuacha familia kuwa tegemezi”Alisema
Afisa Mfawidhi huyo alisema shughuli za usalama sio jambo la mtu mmoja bali ni watu wote hivyo lazima wahakikisha wanazingitia sheria za usalama ikiwemo kuvaa majaketi ya kujiokolea "life jacket" ili yaweze kuwasaidia pindi wanapokumbana na dhoruba baharini waweze kujiokoa.
“Lakini pia kuhakikisha tunakuwa tunazingatia usalama tuwapo majini moto unawaka kutokana na mafuta hauwezi kuuzima na maji ni lazima uhakikisha unatumia mchanga au poda maalumu “Alisema
Hata hivyo alisema ni muhimu na vizuri kwa wenye vyombo vinavyotumika kwa ajili ya shughuli za uvuvi wanakuwa na watu wenye ujuzi na kufanya kazi za majini ikiwemo wajibu wa mmiliki kutii sheria bila shuruti kuhakikisha usalama wake.
Hata hivyo Afisa Mfawidhi huyo aliwataka kuhakikisha kabla hawajaingia majini kuendelea na shughuli zao lazima wawe na cheti kutoka kwenye Shirika hilo ambavyo vinawaruhusu kufanya kazi majini.
“Lakini suala jingine sheria imemuelekeza Afisa Uvuvi asipope leseni ya uvuvi mpaka awe amepata cheti cha Shirika la TASAC cha kuruhusiwa kufanya kazi majini ”Alisema
Friday, April 8, 2022
MOI WAZIDI KUFANIKIWA UPASUAJI UBONGO BILAKUFUNGUA FUVU.
WAGONJWA wanne wamefanyiwa upasuaji mkubwa wa ubongo bila kufungua fuvu la kichwa katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI), ikiwa ni kambi ya wiki moja kati ya madaktari wazawa na madaktari kutoka Hospitali ya Ramaiah nchini India.
Tangu kuanza kwa huduma hiyo Januari 2021 hadi sasa, jumla ya wagonjwa 165 wamefanyiwa upasuaji huo ambao umefanikiwa kwa asilimia 100.
Akizungumza leo Aprili 8, 2022, mara baada ya upasuaji wa mgonjwa wa nne uliochukua dakika 30, Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dk. Respicious Boniface amesema, wameingia mkataba na Hospitali ya Ramaiah iliyoko India, ili wataalamu wa ndani wajifunze zaidi kutumia mashine ya Agio Suite.
Amesema upasuaji huo umekuwa na mafanikio makubwa, ambapo unachukua muda mfupi mgonjwa kupona.
"Lazima tuipe pongezi serikali, kwani lengo lake ni kuhakikisha matibabu yote bingwa na bobezi yanapatikana MOI, kila matibabu yanahitaji upasuaji, hivyo kwa sasa tunafanya.
Alieleza kuwa serilikali ilitoa Sh bilioni 7.9 kwa ajili ya kujenga chumba hicho na kununua mashine.
Amesema kama mgonjwa hana hali mbaya, anafanyiwa akiwa anajua, huku akiongea na watoa huduma wakati wa upasuaji ambapo unachukua dakika 30 hadi 35.
"Ili kutumia ipasavyo upasuaji huo lazima tuwajengea uwezo madaktari wetu, hivyo wamekuja kufundisha wataalamu wetu na tumeingia makaliano na watakuja kila mara tupate uwezo wa kutumia mashine hiyo,"alibainisha.
Kuhusu gharama Dk. Respicious alisema, upasuaji nje ya nchi inategemea na hali ya mgonjwa kuanzia Sh milioni 30 hadi Sh milioni 60 na ndani ni Sh milioni 4 hadi Sh milioni 12.
Daktari bingwa wa mifupa, ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu, John Mtei amesema mafunzo hayo yamewasaidia sana katika kugundua matatizo ya mishipa ya fahamu kwa wagonjwa.
Aliongeza kuwa yameongeza ujuzi, awali walikuwa hawafanyi mara kwa mara, lakini sasa wanafanya wenyewe kwa kuweza kugundua matatizo mapema.
“Wakifika mapema watapata matibabu haraka, mashine inatibu, inachunguza imesaidia kupata vitu vingi na tumejifunza teknolojia mpya na bado tunajifunza,"amesema
Kwa upande wake mgonjwa Hafidhi Said, mkazi wa Singida aliyefanyiwa upasuaji huo wa kichwa bila kufungua fuvu amesema, sasa afya yake imeimarika na kuwashukuru madaktari waliofanikisha upasuaji huo.
"Nilikuwa na tatizo kichwani, lakini baada ya huduma hii sasa naendelea vizuri, nawashukuru madaktari walionihudumia, naamini nitapona kabisa, kwani mwanzo ilikuwa inafikia wakati napoteza fahamu, lakini sasa nipo sawa,"amesema
SOKO LA KARUME LAUNGUA TENA
VIBANDA 33 vimeteketea, baada ya kuzuka moto katika soko la Karume upande wa Uwanja wa Karume, ambapo wamiliki wake ni watu wenye ulemavu.
Akizungumza baada ya kufika katika eneo hilo, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Ng'wilabuzu Ludigija alisema taarifa ya tukio hilo alipata saa 11 alfajiri, ambapo vibanda hivyo vinauza mabegi.
Alisema kutokana na tukio hilo ataunda timu ya uchunguzi ambayo itafanya kazi kwa siku tano na itatoa taarifa ili kuruhusu shughuli za wafanyabiashara hao kuendelea.
" Zipo taarifa kuna mwananchi anayeunganisha umeme kwa wafanyabiashara kinyume na taratibu, hivyo naagiza Jeshi la Polisi limsake au ajisalimishe," alisema.
Alisema hata hivyo timu atakayoiteua ikifanya uchunguzi itatoa maelezo ya kina kuhusu mtu huyo, ili kujua kama ana kibali kutoka Tanesco ama vinginevyo.
" Inasemekana mtu huyo mara kwa mara anakuwa akizuiwa, wafanyabiashara tujiepushe kuruhusu watu wasio na mamlaka ya kuunganisha umeme," alisema.
Awali Mwenyekiti wa Wenye Ulemavu katika soko hilo, Juma Malecha, alimweleza mkuu huyo wa wilaya kuwa wameshatoa taarifa za mtu anayeunganishia wateja umeme, anayejulikana kama Mpemba kwa Tanesco kwa kuwa walikuwa na wasiwasi kuhusu ujuzi alionao.
" Mpemba au Mzee Shaha jana (juzi), alizuiwa kusambaza umeme. Hapa kuna tatizo tutakaa na Tanesco kuona kwa nini wamemrudisha," alisema.
Mwenyekiti huyo ambaye naye ameunguliwa na kibanda chake cha vinywaji na mabegi, alisema kama kiongozi alikataa mtu huyo asiruhusiwe kuingizia wafanyabiashara umeme.
Alisema kabla ya moto huo kuwaka, umeme ulikuwa umekatika uliporudi ndio moto huo ukatokea.
Alisema aliruhusu kwa walinzi kuvunja baadhi ya vibanda kuokoa mali na kuzuia moto usisambae zaidi na kwamba baadhi ya mabegi yaliokolewa, lakini pia kulikuwa na watu wasio waaminifu, ambapo Polisi walifika na kudhibiti hali.
Thursday, April 7, 2022
ROSTAM AZIZ MMILIKI MPYA TIGO, ZANTEL
Mfanyabiashara maarufu nchini, Rostam Aziz ni miongoni mwa wamiliki wa kampuni kubwa ya simu tarajiwa sokoni ya Telmo Tanzania.
Telmo inachukua nafasi ya Tigo na Zantel ambazo zilikuwa zinamilikiwa na Millicom Group kabla ya kununuliwa na Kampuni ya Madagascar, Axian Group (Axian Telecom).
Juzi kampuni ya Millicom International Cellular ilitangaza kukamilika uuzaji na uhamisho wa shughuli zake nchini Tanzania kwenda kwa kampuni mpya ya Axian ambayo itarithi mambo yote, yakiwemo madeni.
Kwa uhamisho huo, Millicom International Cellular imepata fedha taslimu Dola za Kimarekani milioni 100 (Sh233 bilioni).
“Leo hii Tigo ni mtoa huduma mkubwa wa internet kwa wateja, biashara na Serikali katika nchi za Amerika Kusini ambako huduma hizo bado ziko chini. Kwa tangazo la leo tumekamilisha biashara zetu Afrika, tumefunga ukurasa katika historia lakini tumefungua mwingine,” alisema Mauricio Ramos, ofisa mtendaji mkuu wa Millicom.
Juzi hiyohiyo, Kampuni ya Axian Telecom ilieleza kuwa kwa kushirikiana na Rostam wamekamilisha kuinunua Kampuni ya MIC Tanzania Public Limited Company (Tigo na Zantel), hivyo kupanua shughuli za kampuni ya Axian ambayo tayari ipo katika mataifa manane ya Afrika.
“Kwa kuitwaa MIC Tanzania plc, Aaxian Telecom inaanza ukurasa mpya Tanzania. Tunayo furaha kuanza safari hii ya kusisimua na wenzetu hapa na tunaamini kwa pamoja tutafanikisha mambo makubwa na kuchangia katika ulimwengu wa kidijitali,” alisema Hassanein Hiridjee, mwenyekiti wa Axian Telecom.
Hiridjee alitoa shukrani kwa Serikali ya Tanzania na ya Zanzibar kwa kufanikisha mchakato huo.
Alielezea uzoefu wa Rostam katika sekta ya mawasiliano nchini na kwa kuwa ndiye mwenyekiti ajaye wa kampuni hiyo, atatoa mwongozo mzuri kwa ajili ya mfumo mzima wa sekta ya mawasiliano ya simu nchini.
“Tulipoanza safari yetu ya mawasiliano zaidi ya miaka 20 iliyopita, suala lilikuwa kuunganisha watu, tulikuwa tunapambana kujenga mtandao, hususan katika maeneo ya vijijini ili Watanzania wenzetu wafurahi kuunganishwa.
“Kwa kushirikiana na Axian tutaongeza ushiriki wa dijitali, tukijikita zaidi kutoa suluhisho kwa Watanzania na wafanyabiashara,” alisema Rostam, ambaye ni mwenyekiti wa MIC Tanzania plc.
Rostam amewahi kuwa mwanahisa katika Kampuni ya Vodacom Tanzania kabla ya kuuza hisa zake (asilimia 35) zilizokuwa zikisimamiwa na kampuni yake ya uwekezaji ya Mirambo Holdings.
Kampuni ya Mirambo ilikuwa imesajiliwa Tanzania ikimilikiwa na kampuni ya East Africa Investment (Mauritius) iliyosajiliwa katika Jamhuri ya Shelisheli.
Kwa mara ya kwanza Rostam aliuza sehemu ya hisa zake Aprili 2014. Mwaka huo, aliuza asilimia 17.2 ya asilimia 35 alizokuwa anamiliki katika Vodacom Group kwa Dola za Marekani milioni 240 (Sh 557.28 bilioni).
MRADI WA MAJITAKA WA EURO MILIONI 5.3 KUJENGWA MKOANI MWANZA
Na Mohamed Saif- Mwanza
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) kupitia Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC) inatarajia kutekeleza ujenzi wa mradi wa miundombinu ya majitaka na usafi wa mazingira wenye thamani ya Euro Milioni 5.3 kwa lengo la kupunguza uchafuzi wa Ziwa Victoria.
Mradi huo unafadhiliwa kwa ushirikiano wa Serikali ya Tanzania, Serikali ya Ujerumani kupitia Benki yake ya Maendeleo ya KfW na Umoja wa Ulaya (EU) chini ya uratibu wa LVBC kupitia programu ya Pamoja ya Usimamizi na Uendelezaji wa Rasilimali za Maji katika Bonde la Ziwa Victoria (LVB-IWRM).
Hayo yalibainika hivi karibuni Jijini Mwanza katika kikao kilichoshirikisha wadau kutoka MWAUWASA, Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria na ujumbe kutoka Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW) ukiongozwa na Meneja anayesimamia miradi Afrika Mashariki na Umoja wa Afrika, Martina Maurer.
Akizungumza katika kikao hicho, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA, Mhandisi Leonard Msenyele alisema ufadhili huo uliweka vipaumbele mbalimbali vyenye nia ya uhifadhi wa mazingira kwa miji inayozunguka Ziwa Victoria kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
“Mradi utawezesha ukarabati na upanuzi wa mtandao wa majitaka kwa takriban kilomita 14.4 sambamba na kuunganisha kaya 1,600, uboreshaji vituo vya kusukuma majitaka na ununuzi wa vifaa vya usimamizi wa Mfumo wa Majitaka yakiwemo magari ya kuondoa taka majumbani,” alibainisha Mhandisi Msenyele.
Mhandisi Msenyele alisema ufadhili huo unafuatia ushirikiano madhubuti baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan na mataifa ya nje. "Wengi ni mashahidi, mnaona namna ambavyo Rais wetu mpendwa Mama Samia Suluhu Hassan anavyoweka msisitizo kwenye suala la ushirikiano wa kimataifa," alisema Mhandisi Msenyele.
Alisema kukamilika kwa mradi huo kutaleta manufaa makubwa kwenye utunzaji wa Mazingira hususan kupunguza uchafuzi wa Ziwa Victoria. "Mradi huu utasaidia kuwaondolea adha wananchi ya kujaa mara kwa mara kwa mashimo ya vyoo na hii itapunguza uchavuzi wa Ziwa letu," alisema Mhandisi Msenyele.
Kwa upande wake kiongozi wa ujumbe huo ambaye pia ni Meneja wa Benki ya KfW upande wa Afrika, Martina Maurer alisema mradi umelenga kupunguza uchafuzi wa Ziwa Victoria hususan unaotokana na utiririshaji ovyo wa majitaka.
Akielezea kuhusiana na ziara yao hiyo ya siku moja Mkoani Mwanza, Maurer alisema imelenga kujionea eneo la mradi na kujadili namna bora ya utekelezwaji wake.
"Tunatarajia kujifunza mengi kuhusu namna mnavyotekeleza miradi yenu hususan ya utunzaji wa mazingira (uondoshaji wa majitaka) sambamba na kujadili changamoto zinazowakabili kwenye utekelezaji wa miradi kwa ufumbuzi wa pamoja na pia kubaini maeneo zaidi tunayoweza kushirikiana," alisema Maurer.
Akizungumzia utekelezaji wa mradi, Kaimu Meneja Ufundi wa MWAUWASA, Mhandisi Salim Lossindilo alitaja maeneo yatakayonufaika na mradi huo kuwa ni Igogo, Kirumba, Mwaloni, Nyamanoro, Kitangiri na Pasiansi.
Mhandisi Lossindilo vilevile alitaja maeneo kadhaa ya ushirikiano ikiwemo upanuzi wa miundombinu ya majitaka kwenye eneo linalozungukwa na Mto Mirongo ambapo alisema wanatarajia kuunganisha wananchi wapatao 100,000 na mfumo wa majitaka ili kupunguza uchafuzi wa mto huo.
"Tumeandaa maandiko matano ya miradi itakayonufaisha Wilaya za Ilemela na Nyamagana yenye lengo la kutunza Ziwa Victoria na inashirikisha Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Manispaa ya Ilemela, Bodi ya Bonde la Ziwa Victoria pamoja na MWAUWASA,” alibainisha Mhandisi Lossindilo
Ujumbe huo ulipata fursa ya kutembelea maeneo yatakayonufaika na mradi huo wa Uwekezaji wa Kipaumbele cha Juu (HPI-areas), mabwawa ya majitaka ya Butuja na mradi rahisi wa uondoshaji majitaka maeneo ya milimani (Simplified Sewerage System).
Kwa nyakati tofauti ujumbe huo uliipongeza MWAUWASA kwa hatua mbalimbali inazochukua katika kukabiliana na uchafuzi wa mazingira na hususan wa maeneo yanayozunguka Ziwa Victoria.
Wednesday, April 6, 2022
IGP SIRRO APANGUA MAKAMANDA WA POLISI.
Taarifa iliyotolewa leo Jumatano Aprili 6, 2022 na msemaji wa jeshi hilo, David Misime imeeleza kuwa aliyekuwa Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma, Kamishna Msaidi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Onesmo Lyanga amehamishiwa Makao Makuu ya Polisi, huku nafasi yake ikichukuliwa na aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Unguja, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Martin Otieno.
“Aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Daniel Shillah amehamishwa kwenda kuwa kamanda wa polisi mkoa wa Kaskazini Unguja” imeeleza taarifa hiyo.
Aidha, aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Mwanza (RCO), Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Faustine Mafwele amehamishwa kwenda kuwa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Kanda Maalum ya Dar es Salaam (ZCO).
“Aliyekuwa Naibu Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (D/RCO) mkoa wa Mwanza Mrakibu Mwandamnizi wa Polisi (SSP) John Lwamlema anakuwa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Mwanza (RCO)” imeeleza taarifa hiyo
MFUMUKO WA BEI WAFIKIA ASILIMIA 3.7
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema katika mwaka 2021, mfumuko wa bei ulikua kwa wastani wa asilimia 3.7 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 3.3 mwaka 2020.
Majaliwa amezungumza hayo leo Jumatano Aprili 6, 2022 katika hotuba ya Maombi ya Makadilio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2022/23 katika mkutano wa bunge Jijini Dodoma.
Waziri Mkuu amesema kuongezeka kwa mfumuko wa bei kulichangiwa na sababu mbalimbali ikiwemo atahari za Uviko-19, kuongezeka kwa gharama za uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa bidhaa na huduma, kupungua kwa upatikanaji wa mazao ya chakula katika baadhi ya masoko ya ndani kutokana na mabadiliko ya tabianchi.
Amesema mfumuko huo ulikuwa ndani ya lengo la muda wa kati ya asilimia 3 – 5 ambapo wigo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki usiozidi asilimia 8 na ndani ya wigo 17 wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika wa kati ya asilimia 3 - 7.
POLISI WACHUNGUZA MABAKI YA MIILI ILIYOOKOTWA PORINI.
JESHI la Polisi mkoani Tabora linachunguza kubaini mafuvu na masalia ya miili ya binadamu iliyokutwa katika pori la Uyogo wilayani Urambo.
Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Richard Abwao alisema mwili wa mtu ulikutwa kwenye eneo hilo na kwamba masalia ya miili na mifupa imepelekwa kwa Mkemia Mkuu kwa ajili ya uchunguzi.
Abwao alisema jeshi hilo linaendelea na msako kukamata watu waliofanya mauaji hayo na kuacha mabaki ya mifupa na mafuvu.
“Tunafanyia uchunguzi juu ya masalia hayo na kubaini ni nini chanzo cha mauaji hayo yaliyosababisha mtu au watu kutupwa katika pori la Uyogo na kuutupa mwili wa mtu ambaye jina lake halijafahamika ni nani na anatokea wapi kwenye maeneo ya Urambo,” alisema Kamanda Abwao.
Hivi karibuni, iliripotiwa taarifa juu ya kupatikana mafuvu ya watu katika pori lililopo Kata ya Uyogo.
Awali, wananchi walilalamikia upotevu wa ndugu zao na mmoja alibainika kupotea katika kitongoji cha Kitega Uchumi, Kata ya Urambo na baadaye masalia ya mwili na nguo zilitambuliwa na ndugu zake na kulazimika kumzika katika eneo hilo.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Kasela, Kata ya Uyogo, Tomas Petro alisema awali walibaini masalia ya watu waliokufa katika kisima kimoja kilichopo karibu na pori hilo ndipo jeshi la polisi lilifika kwa ajili ya hatua za kiusalama.
Diwani wa Kata ya Songambele, Aliya Kafwenda alisema wameendelea kuimarisha ulinzi na usalama si kwa kata hiyo peke yake bali na nyingine za jirani.
Tuesday, April 5, 2022
SH93.1 BILIONI ZATUMIKA KWENYE MIRADI YA MAENDELEO IRINGA
Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mohamed Hassan Moyo akiongea na wazee Pamoja na viongozi wa dini wa Wilaya hiyo juu ya miradi ya maendeleo yenye thamani ya Jumla ya sh. 93.1 bilioni imetekelezwa katika Wilaya ya Iringa Kwa kipindi Cha mwaka mmoja tangu Serikali ya Awamu ya Sita ilipoingia madarakaniBaadhi ya wazee Pamoja na viongozi wa dini wa Wilaya ya Iringa wakimsikiliza mkuu wa wilaya ya hiyoMohamed Hassan Moyo akielezea mafanikio ya mwaka mmoja wa Rais kwenye wilaya ya IringaBaadhi ya wazee Pamoja na viongozi wa dini wa Wilaya ya Iringa wakimsikiliza mkuu wa wilaya ya hiyoMohamed Hassan Moyo akielezea mafanikio ya mwaka mmoja wa Rais kwenye wilaya ya Iringa
Na Fredy Mgunda,Iringa.
MIRADI ya maendeleo yenye thamani ya Jumla ya sh. 93.1 bilioni imetekelezwa katika Wilaya ya Iringa Kwa kipindi Cha mwaka mmoja tangu Serikali ya Awamu ya Sita ilipoingia madarakani.
Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mohamed Moyo Akizungumza na wazee Pamoja na viongozi wa dini wa Wilaya hiyo Mkoani Iringa alisema kiasi hicho Cha fedha kilielekezwa katika miradi mbalimbali ikiwemo ya Afya, Elimu, miundombinu ya barabara, maji na umeme.
Katika kikao hicho Mkuu wa Wilaya alisema Serikali iliyochini ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha wazee wanapata unafuu wa Matibabu Bure Jumla ya Wazee 793 wamepatiwa vitambulisho ili kuwaondoshea Changamoto ya matibabu.
Moyo alisema kuwa Sh 93.1 bilioni zimetumika katika miradi mbalimbali ya maendeleo wilayani Iringa ikiwemo ujenzi wa barabara ya Kihesa Kilolo – Igumbilo itakayosaidia kupunguza msongamano wa magari mjini.
Alisema kwa sasa magari yote yanapita katikati ya mji na kusababisha msongamano mkubwa kutokana na ukosefu wa barabara mbadala.
“Ikitokea roli likapata ajali mlima wa Ipogoro na kuziba barabara hali lazima iwe tete, lakini Serikali imetoa Sh7.75 bilioni kwa ajili ujenzi wa barabara hii,” alisema.
Moyo alisema shughuli zinazofanyika kwa sasa ni ujenzi wa madaraja na barabara kwa mita 450.
Moyo alisema fedha nyingine zimetumika kwenye kuboresha miradi ya elimu, afya, ujenzi wa uwanja wa ndege, machinjio ya kisasa, sekta ya umeme na biashara.
Aidha mkuu wa wilaya ya IringaMohamed Hassan Moyo alisema kuwa katika sekta ya afya walipata zaidi ya bilioni 5 ambazo zimetumika katika ujenzi ujenzi wa Hospitali,vituo vya afya na zahanati.
Alisema kuwa kiasi cha zaidi ya bilioni 2 zilitumika katika sekta ya elimu msingi kwenye ujenzi wa madarasa,ofisi za walimu,nyumba za walimu na vyoo wakati zaidi ya kiasi cha bilioni 4 zilitumika katika kuboresha miundombinu ya majengo ya shule za sekondari ambapo walitumia katika ujenzi wa madarasa,ofisi za walimu,nyumba za walimu na vyoo.
Moyo alisema kuwa mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania samia Suluhu Hassan ameboresha sekta zote katika wilaya ya Iringa ambapo ametoa kiasi bilioni 93.1 katika sekta za afya,elimu,maendeleo ya jamii,maji,umeme,biashara na mapato,usafiri,ujenzi na barabara
Alisema kuwa kwa kiasi kikubwa fedha hizo zimechochea ukuaji wa uchumi na kuleta maendeleo kwa wananchi wa wilaya ya Iringa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Manispaa ya Iringa, Said Rubeya alisema kazi zilizofanyika zitasaidia kuongeza kasi ya maendeleo kwenye mji huo.
“Tunaona kwa macho kazi zilizofanyika, niipongeze Serikali lakini nikupongeze mkuu wa wilaya kwa kuzungumza haya mbele ya wazee. Vijana wanaweza kukimbia lakini wazee wanaijua njia, tuwasikilize,” alisema.
Kazi kubwa Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akiifanya ndani na mwaka mmoja amefanya mambo mengi Sana na akija Iringa tutampongeza tena-Said Rubeya Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Iringa mjini
MWISHO.