ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Thursday, April 7, 2022

ROSTAM AZIZ MMILIKI MPYA TIGO, ZANTEL


Mfanyabiashara maarufu nchini, Rostam Aziz ni miongoni mwa wamiliki wa kampuni kubwa ya simu tarajiwa sokoni ya Telmo Tanzania.

Telmo inachukua nafasi ya Tigo na Zantel ambazo zilikuwa zinamilikiwa na Millicom Group kabla ya kununuliwa na Kampuni ya Madagascar, Axian Group (Axian Telecom).

Juzi kampuni ya Millicom International Cellular ilitangaza kukamilika uuzaji na uhamisho wa shughuli zake nchini Tanzania kwenda kwa kampuni mpya ya Axian ambayo itarithi mambo yote, yakiwemo madeni.

Kwa uhamisho huo, Millicom International Cellular imepata fedha taslimu Dola za Kimarekani milioni 100 (Sh233 bilioni).

“Leo hii Tigo ni mtoa huduma mkubwa wa internet kwa wateja, biashara na Serikali katika nchi za Amerika Kusini ambako huduma hizo bado ziko chini. Kwa tangazo la leo tumekamilisha biashara zetu Afrika, tumefunga ukurasa katika historia lakini tumefungua mwingine,” alisema Mauricio Ramos, ofisa mtendaji mkuu wa Millicom.

Juzi hiyohiyo, Kampuni ya Axian Telecom ilieleza kuwa kwa kushirikiana na Rostam wamekamilisha kuinunua Kampuni ya MIC Tanzania Public Limited Company (Tigo na Zantel), hivyo kupanua shughuli za kampuni ya Axian ambayo tayari ipo katika mataifa manane ya Afrika.

ADVERTISEMENT

“Kwa kuitwaa MIC Tanzania plc, Aaxian Telecom inaanza ukurasa mpya Tanzania. Tunayo furaha kuanza safari hii ya kusisimua na wenzetu hapa na tunaamini kwa pamoja tutafanikisha mambo makubwa na kuchangia katika ulimwengu wa kidijitali,” alisema Hassanein Hiridjee, mwenyekiti wa Axian Telecom.

Hiridjee alitoa shukrani kwa Serikali ya Tanzania na ya Zanzibar kwa kufanikisha mchakato huo.

Alielezea uzoefu wa Rostam katika sekta ya mawasiliano nchini na kwa kuwa ndiye mwenyekiti ajaye wa kampuni hiyo, atatoa mwongozo mzuri kwa ajili ya mfumo mzima wa sekta ya mawasiliano ya simu nchini.

“Tulipoanza safari yetu ya mawasiliano zaidi ya miaka 20 iliyopita, suala lilikuwa kuunganisha watu, tulikuwa tunapambana kujenga mtandao, hususan katika maeneo ya vijijini ili Watanzania wenzetu wafurahi kuunganishwa.

“Kwa kushirikiana na Axian tutaongeza ushiriki wa dijitali, tukijikita zaidi kutoa suluhisho kwa Watanzania na wafanyabiashara,” alisema Rostam, ambaye ni mwenyekiti wa MIC Tanzania plc.

Rostam amewahi kuwa mwanahisa katika Kampuni ya Vodacom Tanzania kabla ya kuuza hisa zake (asilimia 35) zilizokuwa zikisimamiwa na kampuni yake ya uwekezaji ya Mirambo Holdings.

Kampuni ya Mirambo ilikuwa imesajiliwa Tanzania ikimilikiwa na kampuni ya East Africa Investment (Mauritius) iliyosajiliwa katika Jamhuri ya Shelisheli.

Kwa mara ya kwanza Rostam aliuza sehemu ya hisa zake Aprili 2014. Mwaka huo, aliuza asilimia 17.2 ya asilimia 35 alizokuwa anamiliki katika Vodacom Group kwa Dola za Marekani milioni 240 (Sh 557.28 bilioni).

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.