ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Friday, April 8, 2022

SOKO LA KARUME LAUNGUA TENA

 


VIBANDA 33 vimeteketea, baada ya kuzuka moto katika soko la Karume upande wa Uwanja wa Karume, ambapo wamiliki wake ni watu wenye ulemavu.


Akizungumza baada ya kufika katika eneo hilo, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Ng'wilabuzu Ludigija alisema taarifa ya tukio hilo alipata saa 11 alfajiri, ambapo vibanda hivyo vinauza mabegi.


Alisema kutokana na tukio hilo ataunda timu ya uchunguzi ambayo itafanya kazi kwa siku tano na itatoa taarifa ili kuruhusu shughuli za wafanyabiashara hao kuendelea.


" Zipo taarifa kuna mwananchi anayeunganisha umeme kwa wafanyabiashara kinyume na taratibu, hivyo naagiza Jeshi la Polisi limsake au ajisalimishe," alisema.


Alisema hata hivyo timu atakayoiteua ikifanya uchunguzi itatoa maelezo ya kina kuhusu mtu huyo, ili kujua kama ana kibali kutoka Tanesco ama vinginevyo.


" Inasemekana mtu huyo mara kwa mara anakuwa akizuiwa, wafanyabiashara tujiepushe kuruhusu watu wasio na mamlaka ya kuunganisha umeme," alisema.


Awali Mwenyekiti wa Wenye Ulemavu katika soko hilo, Juma Malecha, alimweleza mkuu huyo wa wilaya kuwa wameshatoa taarifa  za mtu anayeunganishia wateja umeme, anayejulikana kama Mpemba kwa Tanesco kwa kuwa walikuwa na wasiwasi kuhusu ujuzi alionao.


" Mpemba au Mzee Shaha jana (juzi), alizuiwa kusambaza umeme. Hapa kuna tatizo tutakaa na Tanesco kuona kwa nini wamemrudisha," alisema.


Mwenyekiti huyo ambaye naye ameunguliwa na kibanda chake cha vinywaji na mabegi, alisema kama kiongozi alikataa mtu huyo asiruhusiwe kuingizia wafanyabiashara umeme.


Alisema kabla ya moto huo kuwaka, umeme ulikuwa umekatika uliporudi ndio moto huo ukatokea.


Alisema aliruhusu kwa walinzi kuvunja baadhi ya vibanda kuokoa mali na kuzuia moto usisambae zaidi na kwamba baadhi ya mabegi yaliokolewa, lakini pia kulikuwa na watu wasio waaminifu, ambapo Polisi walifika na kudhibiti hali.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.