ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Friday, April 8, 2022

MOI WAZIDI KUFANIKIWA UPASUAJI UBONGO BILAKUFUNGUA FUVU.

 


WAGONJWA wanne wamefanyiwa upasuaji mkubwa wa ubongo bila kufungua fuvu la kichwa katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI), ikiwa ni kambi ya wiki moja kati ya madaktari wazawa na madaktari kutoka Hospitali ya Ramaiah nchini India.


Tangu kuanza kwa huduma hiyo Januari 2021 hadi sasa, jumla ya wagonjwa 165 wamefanyiwa upasuaji huo ambao umefanikiwa kwa asilimia 100.


Akizungumza leo Aprili 8, 2022, mara baada ya upasuaji wa mgonjwa wa nne uliochukua dakika 30, Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dk. Respicious Boniface amesema, wameingia mkataba na Hospitali ya Ramaiah iliyoko India, ili wataalamu wa ndani wajifunze zaidi kutumia mashine ya Agio Suite.


Amesema upasuaji huo umekuwa na mafanikio makubwa, ambapo unachukua muda mfupi mgonjwa kupona.


"Lazima tuipe pongezi serikali, kwani lengo lake ni kuhakikisha matibabu yote bingwa na bobezi yanapatikana MOI,  kila matibabu yanahitaji upasuaji, hivyo kwa sasa tunafanya.


Alieleza kuwa serilikali ilitoa Sh bilioni 7.9 kwa ajili ya kujenga chumba hicho na kununua mashine.


Amesema kama mgonjwa hana hali mbaya, anafanyiwa akiwa anajua, huku akiongea  na watoa huduma wakati wa upasuaji ambapo unachukua dakika 30 hadi 35.


"Ili kutumia ipasavyo upasuaji huo lazima tuwajengea uwezo madaktari wetu, hivyo wamekuja kufundisha wataalamu wetu na tumeingia makaliano na watakuja kila mara tupate uwezo wa kutumia mashine hiyo,"alibainisha.


Kuhusu gharama Dk. Respicious alisema, upasuaji nje ya nchi inategemea na hali ya mgonjwa kuanzia Sh  milioni 30 hadi Sh milioni 60 na ndani ni Sh milioni 4 hadi Sh milioni 12.


Daktari bingwa wa mifupa, ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu, John Mtei amesema mafunzo hayo yamewasaidia sana katika kugundua matatizo ya mishipa ya fahamu kwa wagonjwa.


Aliongeza kuwa yameongeza ujuzi, awali walikuwa  hawafanyi mara kwa mara, lakini sasa wanafanya wenyewe kwa kuweza kugundua matatizo mapema.


“Wakifika mapema watapata matibabu haraka, mashine inatibu, inachunguza imesaidia kupata vitu vingi na tumejifunza teknolojia mpya na bado tunajifunza,"amesema


Kwa upande wake mgonjwa Hafidhi Said, mkazi wa Singida aliyefanyiwa upasuaji huo wa kichwa bila kufungua fuvu amesema, sasa afya yake imeimarika na kuwashukuru madaktari waliofanikisha upasuaji huo.


"Nilikuwa na tatizo kichwani, lakini baada ya huduma hii sasa naendelea vizuri, nawashukuru madaktari walionihudumia, naamini nitapona kabisa, kwani mwanzo ilikuwa inafikia wakati napoteza fahamu, lakini sasa nipo sawa,"amesema

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.