KATIKA kuelekea Sikukuu ya Krismasi na mwaka mpya, Serikali imetangaza punguzo la asilimia 33 ya bei ya mbuzi na kondoo waliopo katika Ranchi za Taifa (NARCO) katika msimu huu wa sikukuu ili kuhamasisha wananchi kula nyama na kuongeza wigo wa soko la ndani.
Akitangaza punguzo hilo, Ofisa Masoko wa Narco, Emmanuel Mnzava alisema Serikali imeamua kutoa ofa ya Krismasi na mwaka mpya kwa wananchi wake ambapo mbuzi 3,000 na kondoo 1,000 watauzwa kwa bei ya punguzo.
Alisema bei hiyo itakuwa katika ranchi za Kongwa (Dodoma), Ruvu (Pwani), Mkata (Morogoro), West Kilimanjaro (Kilimanjaro) na Missenyi (Kagera).
Alisema Rais Samia Suluhu Hassan ameamua kutoa ‘ofa’ ya Krismasi na mwaka mpya kwa wananchi wake ambapo ofa hiyo inalenga kuhamasisha ulaji wa nyama ya mbuzi na kondoo hapa nchini na kuongeza soko la bidhaa hiyo ndani ya nchi.
Aliongeza: “Awali mbuzi mmoja katika ranchi hizi alikuwa anauzwa hadi Sh 150, 000 lakini kutokana na punguzo hili sasa watauzwa kwa Sh 120,000 hadi 100,000, kwa mbuzi na kondoo ambaye akichinjwa anatoa kilo 15 hadi 20.”
Ofisa masoko huyo alitaja lengo lingine la kupunguza bei ni kuhamasisha jamii ya Watanzania katika ufugaji wa kisasa na kibiashara wa mbuzi na kondoo ili kukidhi mahitaji ya soko la kigeni pamoja na machinjio na viwanda vya nyama vilivyopo na vinavyoendelea kujengwa nchini.
Alisema takwimu zinaonesha kuwa ulaji wa nyama ya mbuzi na kondoo hapa nchini bado uko chini ikilinganishwa na ulaji wa nyama ya ng’ombe ambao unaongezeka kila mwaka.
Alisema mahitaji ya nyama ya mbuzi na kondoo katika soko la nje ya nchi na machinjio na viwanda vya nyama vilivyopo na vinavyoendelea kujengwa nchini yanaongezeka, hivyo kutoa fursa la soko la bidhaa hiyo kwa wafugaji.
Kwa upande wake, Mkazi wa Chamwino, Ramadhani Kiza alisema ulaji wa nyama ya mbuzi unakuwa chini kutokana na upatikanaji wake kwa kuwa ni adimu na gharama yake ni kubwa, hivyo watu wengi kushindwa kumudu.
Alisema ni vyema serikali ikaingilia kati suala hili kwa kuwahamasisha wafugaji kufuga mbuzi kisasa na kibiashara ili kufanya nyama ya mbuzi iwe inapatikana kila mahali kama ilivyo bidhaa nyingine.
“Tunamshukuru Rais Samia kwa kutushushia bei ya mbuzi na kondoo lakini tunaomba ofa hii isiwe kwa muda mfupi iwe endelevu
ili kila mwananchi awe na uwezo wa kununua na kufurahi na familia yake hasa kipindi hiki ambacho watu wengi wanasherehekea mwaka mpya na Krismasi,” alisema.
Mfanyabiashara wa Soko la Bonanza, Maria Issa aliipongeza serikali kwa kuleta punguzo la bei kwa wakati ambao unahitajika sana na watu.
Alisema sherehe za mwaka mpya na Krismasi wananchi hununua nyama ya ng’ombe na mbuzi kwa ajili ya kusherehekea na ndugu na jamaa zao.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.