ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Tuesday, September 26, 2023

WATOROSHAJI MADINI KUKIONA SERIKALI YAJA NA MBINU MPYA ZAIDI SASA KUTUMIA GPS.

 NA ALBERT G. SENGO/MWANZA

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amewataka maafisa madini wakazi wa mikoa kwa kushirikiana na vyombo vya usalama kuongeza udhibiti wa utoroshaji wa madini sambamba na kufanya kazi kwa kufuata Sheria ya Madini, kanuni zake na miongozo mbalimbali inayotolewa na Serikali hivyo Sekta ya Madini kuongeza mchango wake kwenye Pato la Taifa na kufikia asilimia 10 ifikapo mwaka 2025. Mavunde ameyasema hayo leo Septemba 26, 2023 jijini Mwanza kwenye kikao chake na menejimenti ya Tume ya Madini kilichoshirikisha Wakurugenzi, mameneja na maafisa madini wakazi wa mikoa. Viongozi walioshiriki ni pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Kheri Mahimbali, Kamishna wa Madini Nchini, Dkt. Abdulrahman Mwanga, Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula, Kamishna wa Tume ya Madini, Janet Lekashingo na Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba. Amesema kuwa, Serikali kupitia Wizara ya Madini imeendelea kuweka mikakati mbalimbali ya usimamizi wa Sekta ya Madini ikiwa ni pamoja na uimarishaji wa udhibiti wa utoroshaji wa madini, maboresho ya mfumo wa usimamizi wa Leseni za Madini, biashara ya madini na kufanya tafiti za madini katika maeneo yote nchini kabla ya mwaka 2030 ikiwa ni utekelezaji wa Dira ya Madini ya Mwaka 2030 ya “Madini ni Maisha na Utajiri.” “Kwenye suala la utoroshaji wa madini Serikali haitamfumbia macho mfanyabiashara au mtu yeyote atakayebainika anatorosha madini, mkakati ni kuhakikisha madini yote yanauzwa kupitia masoko ya madini na vituo vya ununuzi wa madini vilivyoanzishwa nchini na Serikali kupata kodi itakayotumika kuboresha Sekta nyingine muhimu,” amesema Mavunde. Katika hatua nyingine, amewataka maafisa madini wakazi wa mikoa kutatua migogoro kwenye shughuli za uchimbaji wa madini badala ya kusubiri kutatuliwa katika ngazi za juu. Aidha, amewataka maafisa madini wakazi wa mikoa kufanya kazi kwa kushirikiana kwa upendo na kuongeza kuwa Wizara ya Madini itaendelea kutatua changamoto zote katika Sekta ya Madini. Pia amewataka maafisa madini wakazi wa mikoa kufanya kazi kwa bidii na ubunifu wa hali ya juu na kusisitiza kuwa utendaji wao utapimwa kupitia matokeo yanayoonekana hususan kwenye maeneo ya ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.