Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), imetoa angalizo kwa wale wanaopenda kutumia vinywaji vya kuongeza nguvu mwilini maarufu 'Energy drinks'.
Imesema katika utafiti wake mpya umebaini unywaji wa vinywaji hivyo kwa wingi
unaweza kuleta madhara kwenye mishipa ya moyo ya kuziba ghafla na hata
kusababisha vifo vya ghafla.
Hivyo, imeonya kuwa mtu asinywe
zaidi ya kopo moja lenye ujazo wa mililita 250 ndani ya saa 24, huku
ikisisitiza kama kuna uwezekano wa kuviepuka, ifanyike hivyo kulinda afya ya
mhusika.
Baadhi ya vinywaji hivyo ndani yake
kuna maji, sukari, ladha, caffein, mitishamba, tauline (amino acid), protini,
vitamini, madini. Inaelezwa kuwa caffeine pamoja na mambo mengine, inafanya
kazi ya kuzuia uzalishwaji wa kichocheo cha mwili kinachohusika na kulala ama
kuhisi uchovu.
Utafiti huo wa kisayansi umehusisha
unywaji wake na matatizo ya moyo na mishipa kuziba ghafla inayowakumba watu wa
rika zote wanaovitumia hivi sasa.
Akizungumza jana jijini Dar es
Salaam, Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo na Mkuu wa Kitengo cha Utafiti na
Mafunzo JKCI, Pedro Palangyo alisema utafiti huo uliochapishwa juzi katika
jarida moja maarufu la kisayansi nchini Marekani, unamhusisha kijana wa
Kitanzania ambaye mshipa wake mkubwa wa moyo uliziba ghafla.
Hata hivyo, alisema miezi ya hivi
karibuni JKCI imekuwa ikipokea vijana wengi hospitalini hapo wanaofika kutibiwa
wakikabiliwa na changamoto mfanano na hizo, huku wakiwa na historia ya kutumia
vinywaji hivyo.
Ongezeko la matumizi
Dk Pedro alisema matumizi ya
vinywaji vya kuongeza nguvu yamekuwa makubwa katika jamii na yanaongezeka huku
vijana wengi wakivitumia si kwa sababu ya kujipa nguvu, bali kwa kupenda ladha
yake.
"Energy drinks husababisha damu
kuwa nzito kuliko inavyopaswa na ikiwa nzito inaweza kusababisha damu kuganda
kama ilivyokuwa katika kisa hiki, kwa hiyo ni muhimu kuendelea kupaza sauti kwa
jamii zetu na kwa wale wanaviotumia ni vizuri wakaacha kabisa," alisema Dk
Pedro.
Alisema takwimu za hivi karibuni za
taasisi hiyo zinaonyesha wanapata wagonjwa wengi wa mishipa kuziba kwa watu
wenye umri mdogo ambao katika hali ya kawaida ya ugonjwa huo umri mdogo ni mtu
yeyote chini ya miaka 45.
Ukubwa wa tatizo
Wanamichezo, wanafunzi na watu
wanaofanyakazi ngumu ndiyo wanaotajwa zaidi kutumia vinywaji hivyo wakiamini
huwaondolea usingizi, uchovu na kuwapa nguvu zaidi.
Wapo wanamichezo ambao hutumia saa
chache kabla ya kuingia mchezoni au mara baada ya kucheza wakiamini itawafanya
kupata nguvu za ziada na kucheza kwa kiwango.
Huku wanafunzi na madereva
wakivitumia siku za mitihani ili kuuondoa usingizi na wanywaji wa pombe kali
aina ya spiriti na whiskey hutumia kuchanganyia.
Hata hivyo, wataalamu walisema iwapo
mwili umechoka na unaulazimisha kwa kutumia visaidizi ina madhara.
"Ni kweli caffein husisimua
mfumo wa fahamu na kumfanya mtumiaji kuhisi kuchangamka na kuondoa uchovu.
Caffein huainishwa kisayansi kama kundi la opiod yaani dawa ya kulevya aina ya
kichangamshi kiwango chake katika vinywaji hivi kinakubalika ni salama kwa
matumizi ya binadamu lakini unapoulazimisha mwili unauchosha zaidi na
unapozidisha lazima upate madhara na hatushauri kuchanganya na pombe kali ina
madhara makubwa," anasema daktari wa bingwa wa magonjwa ya moyo, Enock
Erick.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.