NA ALBERT G.SENGO/MWANZA
Watoto wawili mapacha wamekufa maji baada ya kutumbukia kwenye lambo la maji yaliyokuwa yametuama mita chache kutoka kwenye nyumba yao wakati wanacheza.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Mwanza Wilbrod Mutafungwa amesema tukio hilo lilitokea jumapili ya Tarehe 23.04.2023 majira ya saa 14:00 mchana, huko katika kijiji cha Runele, Kata ya Hungumalwa, Tarafa ya Nyamilama Wilaya ya kwimba.
Taarifa zaidi zinaarifu kuwa watoto hao wawili wa jinsia ya kiume ambao ni Kulwa Jimoku na Doto Jimoku, wote wakiwa na umri wa mwaka mmoja na miezi sita, ambapo wazazi wao ni Jimuku Rozalia, miaka 28 na Avelina Nkwaya, Miaka 20, wote wakulima na wakazi wa kijiji cha Runele walikufa maji wakati wanacheza nje kidogo ya nyumba yao ambapo walitumbukia kwenye lambo la maji lililopo Mita 30 kutoka kwenye nyumba yao.
Kamanda Mutafungwa ameongeza kuwa lambo hilo limetengenezwa na wazazi hao kwa lengo la kuhifadhia maji ya kunyweshea mifugo yao.
Kamanda amekitaja chanzo cha tukio hilo kuwa ni michezo ya watoto na uzembe wa wazazi kutokuwa makini kwa kuangalia watoto hao wadogo wanaohitaji kuwa na uangalizi wa karibu kutokana na umri wao kwani wakati tukio linatokea wazazi hao walikuwa wanaendelea na shughuli za kilimo .
Miili ya marehemu hao Kulwa na Doto imefanyiwa uchunguzi katika Hospitali ya wilaya ya #Kwimba na kukabidhiwa kwa ndugu kwa mazishi.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.