ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Thursday, December 22, 2016

BAN ATOA WITO KWA PANDE ZOTE DRC KUSULUHISHA MGOGORO KWA AMANI..

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeondoka Ban Ki-moon ametoa wito kwa pande zote zinazohusika katika mgogoro wa kisiasa huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kutatua mgogoro huo kwa njia za amani.
Wito huo wa Ban umekuja baada ya watu  zaidi ya 26 kuripotiwa kuuawa katika maandamano yalioyaoanza Jumatatu dhidi ya Rais Kabila baada ya muhula wake wa uongozi kumalizika.
Taarifa ya msemaji wake imemnukuu Katibu Mkuu akizitaka pande zote zinazohusika katika upatanishi na usuluhishi kuafikiana kwa njia ya amani na kujaribu kutatua masuala yanayohusiana na mipango ya mpito kuelekea uchaguzi mkuu kwa mujibu wa katiba ya DRC.
Ban ametoa wito kwa viongozi wa kisiasa kuweka mbele maslahi ya nchi na raia badala ya maslahi yao binafsi.
Amemsihi Waziri Mkuu Samy Badibanga kuchukua hatua madhubuti kwa mujibu wa makubaliano ya kisiasa ya tarehe 18 Oktoba huku akisisitiza umuhimu wa vikosi vya usalama nchini humo kujizuia kuchukua hatua zinazoweza kusababisha vifo kama vile vilivyoripotiwa kwenye mji mkuu Kinshasa.

Ban ameitaka serikali ya Kinshasa  kwa mara nyingine tena kukuza na kulinda haki za binadamu na kuzingatia uhuru wa kimsingi uliotajwa katika Katiba.
Maandamano dhidi ya rais Kabila mjini Kinshasa
Kambi kuu ya upinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imewataka wananchi kutomtambua tena Joseph Kabila kama rais wa nchi hiyo na imewahimiza kuonesha upinzani wao dhidi ya Kabila kwa njia ya amani.
Kiongozi wa chama kikuu cha upinzani cha Union for Democracy and Social Progress (UDPS), Etienne Tshisekedi, ameitaja hatua ya Rais Kabila ya kuwa madarakani kwa awamu ya tatu kuwa ni kinyume cha sheria na kwamba jitihada zake za kutaka kubakia madarakani ni mapinduzi ya kijeshi.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.