Na WMJJWM- New York Marekani
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima amesema Tanzania inatambua umuhimu wa ushiriki wa wanawake kuanzia ngazi ya chini kwenye jamii ambayo itawezesha kupata matokeo chanya yatakayotoa majibu na tija kwa changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa, mazingira na majanga kwa kuzingatia usawa wa jinsia.
Dkt Gwajima ameyasema hayo akiwa jijini New York nchini Marekani katika Mkutano wa Mawaziri ndani ya Mkutano wa mkutano wa 66 wa hali ya wanawake duniani.
Dkt. Gwajima amesisitiza kuwa Tanzania inashiriki kikamilifu kwenye juhudi za kutunza mazingira, kudhibiti mabadiliko ya hali ya hewa na majanga na kwa sababu hiyo imesaini makubaliano mbalimbali ikiwemo azimio la Beijing, azimio la umoja wa mataifa kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa(UNFCC), azimio la Kyoto 1997, ajenda 2030 na CEDAW.
Katika hatua nyingine Dkt. Gwajima amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan ameridhia kuwa kinara wa utekelezaji wa jukwaa la kizazi chenye usawa kwenye eneo la uwezeshaji wa haki za kiuchumi, eneo linalolenga kuwezesha uhakika wa upatikanaji wa chakula, uchumi na maisha bora kwa ujumla.
Waziri Dkt. Gwajima ameongoza ujumbe wa Tanzania New York nchini Marekani kushiriki mkutano wa 66 wa hali ya wanawake duniani uliojumuisha Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Amon Mpanju, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jinsia Mwajuma Magwiza, Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Maendeleo ya Jinsia Badru Abdulnoo na Maafisa wengine wa Wizara
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.