MADHIMISHO ya Siku ya Upandaji Miti Kitaifa na Siku ya Misitu Duniani mwaka 2022 yatafanyika Wilayani Magu, mkoani Mwanza yakiongozwa na Kaulimbiu isemayo 'MTI WANGU, TAIFA LANGU, MAZINGIRA YANGU, KAZI IENDELEE'.
Maadhimisho hayo yatafanyika kwa mara ya kwanza nchini Tanzania yakiwa yameongozwa na malengo makuu mawili ambayo ni kuwakumbusha na kuwahamasisha Watanzania kuhusu umuhimu wa upandaji na utunzaji wa miti kwa ajili ya kuongeza upatikanaji wa bidhaa na huduma za misitu hapa nchini. Akizungumza mbele ya Kamati ya Maandalizi kwa Maadhimisho hayo Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Magu ambaye pia ni Mkuu wa wilaya hiyo Salum Kalli amesema kwake ni neema kubwa sana na akiishukuru Serikali kwa kuipa fursa wilaya yake kwani kwa kipindi kirefu imekuwa na uhitaji wa miti kutokana na uharibifu wa mazingira uliofanyika. Zoezi la upandaji miti wilayani Magu linatarajiwa kuanza siku hiyo ya Jumatatu ya Tarehe 21 March 2022 kuanzia majira ya saa 12 asubuhi hadi saa 6 mchana, likifuatiwa na mkutano utakaotumika kama darasa la kutoa Elimu iliyojikita katika kukumbusha na kuhamasisha umma wa watanzania juu ya umuhimu wa kupanda miti, kuitunza, na kuihifadhi misitu iliyo katika maeneo yao kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho. Kwa kipindi kirefu eneo kubwa la wilaya ya Magu limekuwa kame kutokana na baadhi ya wananchi wake kujihusisha na biashara ya uchomaji mkaa pamoja na uvunaji hovyo wa miti kwaajili ya mbao. Mpaka sasa zaidi ya miti 65,500 imepandwa wilayani humo, huku lengo likiwekwa hadi kufikia tamati ya maadhimisho hayo wilaya iwe imepanda zaidi ya miti laki moja. Maadhimisho hayo ya Siku ya Upandaji Miti Kitaifa ambayo hufanyika Aprili 1 ya kila mwaka sasa yatafanyika Machi 21, 2022 yakiwa yameunganishwa.Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.