Yanga imerejea katika nafasi ya pili jioni hii baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Kagera Sugar FC, mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Mechi hiyo iliyopigwa Uwanja wa Taifa Dar es Salaam, ilimalizika dakika 45 za kwanza kukiwa hakuna timu iliyoweza kuona lango la mwenzake.
Kipindi cha pili kilikuwa na neema kwa Yanga, ambapo mnamo dakika ya 53, Ibrahim alifunga bao la kwanza kwa njia ya penati, baada ya beki wa Kagera kuunawa mpira eneo la hatari.
Yanga walizidi kuamka zaidi haswa kuelekea dakika za mwisho kipindi cha pili, ambapo katika dakika ya 77, Yusuph Mhilu, alifunga bao la pili na kufanya ubao wa matokeo usomeke kwa mabao 2-0.
Kazi nzuri ya Mhilu ilizidi kuzaa matunda tena, ambapo mnamo dakika ya 88, Juma Shemvuni alijifunga, kufuatia kazi nzuri ya Yusuph Mhilu, baada ya kupiga shuti kali ambalo lilisababisha Shemvuni kujifunga.
Mpaka Mwamuzi anapuliza filimbi ya mwisho, Yanga walikuwa mbele kwa mabao 3-0 dhidi ya Kagera Sugar.
Matokeo hayo sasa yameirejesha Yanga mpaka nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara, na kuifanya ibakize alama 3 pekee kuifikia Simba inayoongoza ligi.
Yanga sasa ina pointi 43 ikiwa nafasi ya pili, huku Simba ina alama 46, na Azam imeshuka hadi nafasi ya tatu ikiwa na alama zake 42.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.