Waziri wa Maji, Mhe. Prof. Makame Mbarawa (Mb) akikata utepe kuzindua rasmi mradi wa maji wa Kijiji cha Shilima, Kata ya Kikubiji, Wilaya ya Kwimba, Mkoani Mwanza.
Baadhi ya wananchi waliofika kushuhudia uzinduzi wa mradi wa maji wa Shilima
Waziri wa Maji, Mhe. Prof. Makame Mbarawa (Mb) (mbele katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi waliohudhuria uzinduzi wa mradi wa maji Shilima.
Mamlaka za maji zinazotumia bei za kukadiria (flat rates) kote nchini zimepewa miezi mitatu kuhakikisha zinawafungia dira za maji wateja wao wote ili kila mteja alipe gharama ya maji kwa kiasi alichotumia.
Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa (Mb) alitoa agizo hilo Septemba 14, 2019 alipokuwa akizindua mradi wa maji wa Kijiji cha Shilima Kata ya Kikubiji, Wilaya ya Kwimba Mkoani Mwanza.
Waziri Mbarawa alisema Serikali imetenga Bilioni moja kusaidia mamlaka za maji ambazo hukadiria matumizi ya maji wateja wake badala ya kutumia dira ya maji ili kuepuka kumbebesha mteja mzigo usiyo kuwa wake.
Waziri Mbarawa vilevile ameziagiza mamlaka za maji za mikoa kuhakikisha zinadhibiti upotevu wa maji kwani maji mengi yanapotea kabla ya kufika kwa wananchi sambamba na kuongeza mtandao wa maji ili kuwaunganisha wananchi wengi zaidi.
Akizungumzia mradi wa maji wa Shilima, Profesa Mbarawa alisema ujenzi wake ni utekelezaji wa Sera ya Maji pamoja na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi inayoelekeza kuwapatia huduma ya majisafi na salama kwa asilimia 85 wakazi wote waishio vijijini ifikapo mwaka 2020.
Aliongeza kuwa uzinduzi wa mradi huo ni awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi wa maji katika Vijiji vya Shilima, Mhande na Izizimba.
Alibainisha kwamba mradi wa maji wa Shilima ulianza kutekelezwa mwaka 2013 na ulitakiwa kukamilika katika kipindi cha miezi sita. Hata hivyo, kutokana na udhaifu wa Mkandarasi aliyekuwa anautekeleza pamoja na usimamizi mbovu haukuweza kukamilika kwa wakati.
Waziri Mbarawa aliwapongeza wote walioshiriki kwenye ujenzi wa mradi kwa namna mbalimbali na kwa ushirikiano waliotoa kwa kipindi chote cha ujenzi wake hadi unakamilika kwa wakati kama alivyokuwa ameelekeza.
Akizungumzia ujenzi wa mradi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jijini Mwanza (MWAUWASA) ambaye alikuwa msimamizi mkuu wa ujenzi, Mhandisi Anthony Sanga alisema walizingatia agizo la Waziri Mbarawa na kwamba mradi huo ulikamilka tarehe 25 Agosti, 2019 kabla ya muda uliyokuwa umeelekezwa.
Kwa upande wake Meneja wa RUWASA Wilaya ya Kwimba, Mhandisi Boaz Matundalo alisema kuwa Kijiji cha Shilima kina wakazi wapatao 7,526 ambapo mradi huu wenye magati 35 una uwezo wa kuhudumia wakazi 8.750 ikiwa ni wastani wa watu 250 kwa kila gati.
Waziri Mbarawa tarehe 3 Julai, 2019 akiwa katika ziara ya kikazi Wilayani Kwimba alitoa ahadi ya kukamilisha mradi huo kwa kutumia wataalamu wa ndani kwa kuhakikisha wananchi wa Kijiji cha Shilima wanapata maji katika kipindi cha miezi miwili, yaani hadi kufikia tarehe 3 Septemba, 2019, ahadi ambayo hata hivyo ilikamilika tarehe 25 Agosti, 2019 siku tisa kabla ya tarehe ya makubaliano.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.