ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Monday, March 16, 2026

MVUA MOROGORO YASABABISHA VIFO VINNE

 


Mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Morogoro zimesababisha vifo vya watu wanne katika matukio tofauti, huku wengine wakijeruhiwa baada ya kupigwa na radi.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, SACP Alex Mkama, amesema watu wawili walifariki dunia baada ya kupigwa na radi wakati wa mvua kubwa katika Kijiji cha Kilosa Mpepo wilayani Malinyi.

Amewataja waliofariki kuwa ni Nindi Masele (15) na Marwa Mwanzilwa (2), wote wakazi wa kijiji hicho, waliopoteza maisha usiku wa Machi 13, 2026 wakati mvua kubwa ikiendelea kunyesha.

Aidha, amesema watu wengine wanne wa familia moja walijeruhiwa katika tukio hilo akiwemo Milembe Dase (27), Kulwa Malembe (38), Milembe Samwel (39) pamoja na Ngolo Nchimwe (1), ambao wanaendelea kupatiwa matibabu.

Ndani ya mwezi mmoja uliopita, tukio jingine la radi lilitokea Februari 23 mwaka huu katika Kitongoji cha Mbesi, Kijiji na Kata ya Utengule, Halmashauri ya Mlimba wilayani Kilombero.

Katika tukio hilo, watu wawili Tano Leonard Lunasi (36) na Ngimila Ndombeji Mashana (27), wote wakulima na wakazi wa eneo hilo, walipoteza maisha huku wengine wawili wakijeruhiwa walipokuwa wakirejea nyumbani kutoka matembezini.

Katika tukio jingine, watu wawili Hamis Yahaya Waziri (45), mkulima mkazi wa Kisaye na Nyerere Katebeka Kidagati (50), mfugaji mkazi wa Mkono wa Mara wilayani Morogoro, wamefariki dunia baada ya kusombwa na maji ya mvua.

Kamanda Mkama amesema watu hao walifariki katika kata za Tegetero na Mkambarani walipokuwa wakijaribu kuvuka maeneo yaliyofurika maji lakini walizidiwa nguvu na kusombwa na maji.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment