SHEHENA: Shehena ya mbolea ikiwa katika moja ya maghala yaliyopo mkoani Mbeya tayari kwa matumizi wakati wa msimu wa kilimo.
Mkaguzi wa mbolea Allan Mariki, akikagua ubora wa mbolea katika moja ya ghala la kuhifadhia mbolea ili kuhakikisha kuwa mbolea inayowafikia wakulima imekidhi viwango vya ubora vinavyotakiwa
Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kupitia vyama vya ushirika inawahamasisha wakulima nchini kununua mbolea kwa pamoja kutoka kwa wazalishaji/makampuni yanayoingiza mbolea moja kwa moja badala ya mkulima mmoja mmoja kununua kutoka kwa wafanyabiashara wa kati ili kununua mbolea hiyo kwa bei ya jumla na hivyo kuipata kwa bei ya chini tofauti na kila mkulima akinunua kiasi kidogo cha mbolea.
Wito huo umetolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Uzalishaji wa Ndani na ununuzi wa Mbolea wa Pamoja, Joseph Charos alipokuwa akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya mamlaka hiyo kwenye kikao cha Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka hiyo mwishoni mwa wiki.
Charos alieleza kuwa, Kutokana na bei za mbolea katika soko la dunia kuendelea kuwa juu, bei za soko la ndani pia zimeendelea kupanda. Alisema, kwa mfano, wastani wa bei ya mkulima (Retail price) kwa mbolea ya Urea umepanda kutoka Sh. 53,318 mwezi Desemba, 2020 na kufikia Sh. 104,069 mwezi Desemba, 2021 kwa mfuko wa kilo 50, wakati wastani wa bei ya mbolea ya DAP umepanda kutoka Sh. 66,995 mwezi Desemba, 2020 hadi Sh. 109,179 mwezi Desemba, 2021 kwa mfuko wa kilo 50 sawa na ongezeko la 95% na 63% mtawalia.
Alifafanua kuwa, kwa mujibu wa bei za mbolea zilizokuwa zikitangazwa na soko la dunia katika kipindi cha Julai - Desemba 2021, kwa wastani bei za mbolea zilizoingia nchini zilikuwa nafuu ambapo kwa mbolea ya UREA, bei ya chanzo (FOB) katika soko la dunia kwa mwezi Julai hadi Desemba ilikuwa kati ya dola za marekani 420 hadi 1,000 kwa tani wakati wastani wa bei hadi hapa nchini (CIF Value) kwa mbolea iliyoingia katika kipindi hicho ni kati ya dola za marekani 570 hadi 1,398 kwa tani.
Akielezea kwa upande wa DAP, Charos alisema bei ya chanzo (FOB) katika soko la dunia kwa mwezi Julai hadi Desemba ilikuwa kati ya dola za marekani 550 hadi 912 kwa tani wakati wastani wa bei hadi hapa nchini (CIF Value) kwa mbolea iliyoingia nchini katika kipindi hicho ni kati ya dola za marekani 659 hadi 810 kwa tani.
Kufuatia bei za mbolea kuwa juu kwenye soko la dunia, soko la ushindani nchini limesababisha wafanyabiashara wafanye jitihada za kutafuta mbolea kutoka kwenye vyanzo vyenye bei nafuu ili kupunguza bei ya mbolea kwa wateja wao.
Akihitimisha taarifa yake Charos alisema, Kwa ujumla, bei za mbolea zilizoingia nchini katika kipindi cha Julai - Desemba 2021 zimepanda kwa mbolea zote zikilinganishwa na bei za kipindi kama hiki mwaka 2020/2021.
Aliongeza kuwa, wastani wa bei ya kufikishia mbolea ya DAP hapa nchini (CIF) kwa mwezi Desemba, 2020 ilikuwa dola za kimarekani 362 ikilinganishwa na wastani wa dola za kimarekani 810 kwa mbolea iliyoingia mwezi Desemba, 2021 sawa na ongezeko la 123%, ambapo kwa mbolea ya Urea, bei ya kuifikisha hapa nchini (CIF) kwa mwezi Desemba, 2020 ilikuwa dola za marekani 310 wakati bei ya mbolea iliyoingia chini mwezi Desemba, 2021 ni dola za marekani 1,398 sawa na ongezeko la 350%.
Hata hivyo, mamlaka inaendelea na juhudi za kuwahamasisha wakulima kupitia vyama vya ushirika na wataalam wa kilimo, kutumia mbolea mbadala katika shughuli za kilimo zinazopatikana kwa gharama nafuu na kuwataka kuzingatia ushauri wa wataalam.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.