
ELIZABETH Sylvester maarufu kama Sosomo, mkazi wa Kijiji cha Chudeko, Wilaya ya Songwe, amehukumiwa kifungo cha nje cha miezi 18, baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kumuua mumewe, Ally Masanja, bila kukusudia.
Hukumu hiyo imetolewa na Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songwe, imemhukumu Katika kesi hiyo namba 7304/2026, mshitakiwa alikiri kosa la kuua bila kukusudia kinyume na vifungu vya 195 na 198 vya kanuni ya adhabu, Sura ya 16, kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2023.
Kwa mujibu wa ushahidi uliowasilishwa mahakamani hapo na wakili wa Serikali, Elbariki Mpinga, tukio hilo lilitokea Januari 3, 2026 katika Kijiji cha Chudeko, wilayani Songwe, ambapo mshitakiwa alimchoma mumewe kisu ubavuni wakati wa ugomvi uliotokana na wivu wa mapenzi.
Ilielezwa kuwa ugomvi huo ulizuka baada ya mshitakiwa kumkuta mumewe akiwa nyumbani kwa mwanamke anayedaiwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi.
Hali hiyo iliyoibua ugomvi kati yao watatu hao, hadi kufikia kwenye shambulio hilo lililosababbisha mauti ya mwanaume huyo.
Akisoma hukumu Aprili 21, 2026, Jaji Mfawidhi wa mahakama hiyo, Jaji Gabriel Malata, amesema mahakama imezingatia mazingira ya tukio, ikiwemo hali ya mshtakiwa kabla, wakati na baada ya tukio pamoja na ungamo lake.
Alisema mahakama ilimtia hatiani kwa kosa hilo na kuamua kumpa adhabu hiyo ya kifungo cha nje cha miezi 18 kwa kuzingatia masharti ya kisheria.
Kwa mujibu wa hukumu hiyo, mshitakiwa hataruhusiwa kutenda kosa lolote la jinai katika kipindi hicho, na endapo atakiuka masharti hayo atalazimika kutumikia kifungo hicho gerezani.
Kesi hiyo ni miongoni mwa kesi tatu za mwanzo kutolewa hukumu na Mahakama Kuu Kanda ya Songwe tangu kuanza rasmi kwa shughuli zake za kimahakama Machi 30, 2026.
Awali, Wakili wa utetezi, Moses Mwampashi, aliomba mahakama imuonee huruma mshitakiwa, akieleza kuwa hilo ni kosa lake la kwanza na halikupangwa bali lilitokana na mazingira ya tukio.
Aliongeza kuwa mshitakiwa ana watoto wanne aliowazaa na mumewe,ambao kwa sasa ndiye mtu wa kuwalea na wanamtegemea, hivyo kuiomba mahakama izingatie maslahi yao katika utoaji wa hukumu.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment