Na.Mwandishi Wetu - Ruvuma
Waziri Afya Mheshimiwa Jenista Mhagama amezindua Usambazaji wa Ripoti ya Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI 2022-2023 Mkoani Ruvuma.
Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika Wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma tarehe 29 Novemba, 2024 Waziri Mhagama alieleza mafanikio makubwa yaliyopatikana katika juhudi za kudhibiti maambukizi ya UKIMWI nchini Tanzania ambapo imeelezwa kuwa kiwango cha Maambukizi Mapya kimepungua huku akipongeza juhudu zinazofanywa na Tume ya Kudhibiti UKIMWI Nchini
"Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kiwango cha maambukizi ya UKIMWI nchini kimepungua kwa kiasi kikubwa kutoka asilimia 7 mwaka 2022 hadi asilimia 4.4 mwaka 2023. Aidha, juhudi za kupunguza maambukizi ya mama kwenda kwa mtoto zimezaa matunda, ambapo kiwango cha maambukizi kimepungua kutoka asilimia 18 mwaka 2010 hadi asilimia 8.1 mwaka 2023," alisema Waziri Mhagama
Waziri Mhagama alieleza kuwa mafanikio haya yametokana na juhudi za Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo, sekta binafsi, na jamii katika kuimarisha programu za utoaji elimu, upimaji wa hiari, na matumizi ya dawa za kufubaza makali ya virusi vya UKIMWI (ARVs).
Alisisitiza umuhimu wa kuendelea na juhudi hizi ili kufikia malengo ya kumaliza maambukizi mapya ya UKIMWI, hasa kwa watoto, ifikapo mwaka 2030. Vilevile, aliwahimiza wananchi kuendelea kuchukua hatua za kujikinga na maambukizi na kufuata ushauri wa kitaalamu.
Aidha alitoa wito kwa jamii kuunga mkono mikakati ya kitaifa ya kupambana na UKIMWI ili kuhakikisha maendeleo ya afya ya jamii na uchumi wa taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Mheshimiwa Ummy Nderiananga, amesema Watanzania wamepiga hatua kubwa katika mapambano dhidi ya maambukizi ya Virusi vya UKIMWI (VVU)ambapo asilimia 98 ya Watanzania wanaohitaji dawa za kufubaza makali ya virusi hivyo (ARVs) sasa wanatumia dawa hizo, hatua ambayo imevuka malengo yaliyowekwa kitaifa na kimataifa.
Mhe. Ummy alibainisha kuwa mafanikio haya ni matokeo ya jitihada za serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, ikiwemo utoaji wa elimu ya afya, upimaji wa hiari, na utoaji wa dawa kwa urahisi katika vituo vya afya.
Pia ametumia nafasi hiyo kuhimiza wananchi kuendelea kuchukua hatua za kujikinga na kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kuendelea kutumia dawa kwa walioambukizwa ili kuboresha maisha yao na kupunguza maambukizi mapya.
Serikali inaendelea kuweka mikakati imara kuhakikisha kila Mtanzania anayehitaji huduma za matibabu anazipata kwa wakati.
Maadhimisho ya Wiki ya UKIMWI Duniani yanaadhimishwa Kitaifa mkoani Ruvuma yenye kauli Mbiu isemayo "Chagua Njia Sahihi, Tokomeza UKIMWI"
=MWISHO=
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.