Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli. |
Rais Magufuli ametoa kauli hiyo mbele ya Masheikh, Maimamu na viongozi wa dini ya Kiislamu na baadhi ya viongozi na waumini wa madhehebu mengine mbalimbali ya dini aliowaalika katika futari jana jioni tarehe 14 Juni, 2016 Ikulu Jijini Dar es salaam.
"Kwa niaba ya serikali na mimi mwenyewe na watanzania kwa ujumla, napenda kutumia fursa hii adhimu kuwatakia waislamu wote nchini Tanzania mfungo mwema wa mwezi mtukufu wa Ramadhani, uwe mfungo wa amani na wenye baraka, lakini pia ninamuomba Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema azikubali funga zenu na kuwalipa malipo stahiki.
"Niwaombe ndugu zangu waislamu msisahau kuliombea taifa hili amani, palipo na amani ndipo palipo na maendeleo ya kweli, palipo na amani ndipo biashara itaenda vizuri, palipo na amani hata mahubiri mazuri kwa watu yatasikika vizuri, tulisimamie hili kwa manufaa ya Tanzania" Amesema Rais Magufuli.
Pamoja na kuwaalika watanzania wote kuliombea taifa, Rais Magufuli pia amewahakikishia watanzania wote kuwa serikali yake ipo imara kuhakikisha inailinda na kuidumisha amani iliyopo.
Aidha, Dkt. John Pombe Magufuli ameelezea kufurahishwa kwake na umoja na ushirikiano wa viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini wanaounda kamati za amani za mikoa.
Pia amewataka wafanyabiashara wa vyakula waache kupandisha bei za vyakula hasa vinavyotumika wakati wa mfungo huu wa mwezi mtukufu wa Ramadhani ili kuwawezesha waliofunga kumudu kununua vyakula hivyo.
Katika futari hiyo Rais Magufuli na Mkewe Mama Janeth Magufuli wameungana na viongozi mbalimbali wa dini wakiwemo Kaimu Mufti wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Alhaji Hamid Masoud Jongo, Askofu Mkuu wa Anglikani wa Mkoa wa Dar es salaam Baba Askofu Valentino Mokiwa, na Mke wa Waziri Mkuu Mama Mary Majaliwa na Mwenyekiti wa Wanawake Waislamu Tanzania Hajjat Shamim Khan.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.