Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Dkt Dorothy Gwajima amesema kuwa Serikali haitasita kuwafutia leseni wamiliki wa Vituo Binafsi vya Afya Nchini watakaobainika kuwashawishi watumishi waliopo kwenye taasisi za umma muda wa kazi kwenda kufanya kazi kwenye vituo vyao kinyume na sheria na taratibu za nchi hali inayosababisha kuzorota kwa huduma kwenye taasisi za serikali.
Rai hiyo ameitoa jijini Dar es Salaam leo 03. Desemba 2021 katika ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 22 wa Chama cha Wamiliki wa Vituo vya Binafsi vya Afya Nchini ukihusisha watoa huduma za afya kutoka mataifa mbalimbali. Amesema Wafanyakazi waliopo katika Taasisi za umma kwenda kufanyakazi katika Sekta Binafsi muda wa kazi lazima ifanyike kwa utaratibu mzuri usiathiri huduma za upande mwingine kwani kufanya hivyo sio tu kuwa ni kosa kisheria bali ni kitendo kisicho na utu kwani tunawanyima haki wateja wengine waliofika kupata huduma.
Dkt Gwajima amesema kuwa inakadiriwa 36% ya gharama za uendeshaji inapotea kutokana na kukosa ufanisi katika mifumo ya kiutendaji.
Habari njema ni kwamba ikiwa tutafanya kazi kwa ufanisi na kuokoa 36% ambayo tunapoteza, tunaweza kupunguza gharama ya huduma ya afya kwa 36% ambayo inapotea na hivyo kutoa huduma kwa watu wetu kwa kiwango kikubwa na gharama za huduma kuwa nafuu zaidi ili kuwapunguzia gharama wananchi.
Nitoe Rai kwa watoa huduma binafsi kuwekeza katika teknolojia bunifu zitakazotusidia kuongeza ufanisi wa kiutendaji kwa kupunguza gharama za utoaji huduma za Afya kwa wananchi ili wafurahie matunda ya Taifa lao amesema Dkt.Gwajima
Aidha Dkt Gwajima amesisitiza APHFTA kuendelea kushirikiana na Serikali kuzuia ubadhirifu wa mali za unaofanywa na baadhi ya watendaji wasio waaminifu wa upande wa serikali na sekta binafsi kwa kununua au kuhamisha mali za umma na kuzipeleka kwenye Sekta Binafsi kinyume na utaratibu. Amesema kitendo hiki ni sawa na uhujumu uchumi na kinazorotesha juhudi za Serikali.
"Tanzania imefika mbali sana katika kukidhi mahitaji ya afya ya watu kwa kutambua ukweli kwamba sekta ya afya binafsi ina mengi ya kutoa, na kwamba kwa pamoja tunaweza kukabiliana vyema na mahitaji ya afya ya sasa na ya baadaye ya Watanzania hivyo
tunahitaji ushiriki mkubwa wa sekta binafsi katika utoaji huduma zikiwemo chanjo mbalimbali na ya Uviko 19, huduma za matibabu ya VVU/UKIMWI na kifua kikuu, uzazi wa mpango na Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza" Amesema Dkt Gwajima
Dkt Gwajima amesema kuwa Wizara ya Afya imefurahishwa na kazi ambayo APHFTA inafanya katika Kuzuia Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza (NCDs) na kuzuia magonjwa yasiyoambukiza ambacho kinahusishwa na programu za afya shuleni ni kielelezo kinachotia matumaini kuwa APHFTA ni mshirika muhimu katika mpango wa Kitaifa wa kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza, haswa kupitia programu yake ya shule, ambayo hivi karibuni itapanuliwa kitaifa.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.