ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Tuesday, February 17, 2026

MTUNZI WA TANZANIA YETU MZEE STEVEN HIZZA AFARIKI DUNIA TANGA

 


Mwanamuziki mkongwe nchini Tanzania, Mzee Steven Hizza, aliyepata umaarufu mkubwa kupitia wimbo wa kizalendo wa “Tanzania Yetu Ndiyo Nchi ya Furaha,” amefariki dunia jioni ya Jumatatu, tarehe 16 Februari 2026, katika eneo la Mwanzange, jijini Tanga.

Taarifa za kifo chake zimethibitishwa na watu wa karibu wa familia, wakieleza kuwa msanii huyo mkongwe amefariki akiwa nyumbani kwake Mwanzange, ambako aliishi kwa muda mrefu baada ya kustaafu rasmi jukwaani.

Mzee Hizza anakumbukwa kama miongoni mwa wanamuziki waliotumia kipaji chao kuhubiri uzalendo, mshikamano wa kitaifa na mapenzi kwa nchi. Wimbo wake maarufu wa “Tanzania Yetu Ndiyo Nchi ya Furaha” uliwahi kutamba katika vipindi mbalimbali vya redio na matukio ya kitaifa, ukiimbwa pia mashuleni na katika sherehe za kitaifa kama sehemu ya kuhamasisha ari ya uzalendo kwa vizazi vipya.

Katika historia ya muziki wa Tanzania, Mzee Hizza alijijengea heshima kama msanii wa maadili, aliyeamini kuwa muziki ni chombo cha kuelimisha na kuunganisha jamii. Mbali na wimbo huo maarufu, alishiriki pia katika matamasha ya kitaifa na shughuli za kijamii zilizolenga kuhamasisha amani, umoja na maendeleo.

Wadau wa muziki wanamkumbuka kwa sauti yake ya kipekee na mashairi yenye ujumbe mzito yaliyoakisi uzalendo wa dhati. Kwa miaka mingi, kazi zake zimeendelea kurushwa hewani na kubaki sehemu ya kumbukumbu muhimu ya muziki wa kizazi cha zamani uliobeba maadili na utambulisho wa Taifa.

Mara ya mwisho Mzee Stephen kusikika ilikuwa ni mwaka 2011 alipohojiwa kipindi Tanzania ilipokuwa ikitimiza miaka 50 ya uhuru.

Kifo chake kinaacha pengo kubwa katika tasnia ya muziki wa kizalendo nchini, huku wengi wakiamini kuwa mchango wake utaendelea kuishi kupitia kazi zake zilizogusa mioyo ya Watanzania wengi.

Hadi sasa, taarifa rasmi kuhusu chanzo cha kifo chake pamoja na ratiba ya mazishi zinatarajiwa kutolewa na familia pamoja na viongozi wa tasnia ya muziki nchini.

  • RAIS ATUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI


Wakati huo huo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ametuma salamu zake za rambirambi kwa nguli huyo akisema:-

"Nimepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha Mzee Steven Hiza, nguli wa muziki na mtunzi wa wimbo, “Tanzania Yetu.”


Tunatambua na tutaendelea kuenzi mchango wake mkubwa katika sekta ya muziki, ambapo wimbo wake wa Tanzania Yetu umeipamba nchi yetu, umetukumbusha wajibu wetu kwa Taifa letu, umetuelimisha na kutuburudisha kwa takribani miaka 60 sasa.


Ninawaombea subra na uvumilivu familia, ndugu, jamaa, marafiki na wote walioguswa na msiba huu. Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi. 


Amina.

Nukuu ya Rais wetu mpendwa Mhe.dkt.Samia Suluhu Hassan

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment