MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo, Othman Masoud Othman amesema chama hicho kimeingia katika maridhiano ya kisiasa kwa ajili ya kuimarisha amani na utulivu katika serikali ya umoja wa kitaifa.
Masoud ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, alisema hayo wakati akizungumza na wanachama na wananchi katika mikutano ya hadhara Wilaya ya Kati Unguja na Magharibi katika ziara yake ya kujitambulisha.
“Maridhiano ya kisiasa yamefungua milango ya heri na maelewano ambapo siasa za chuki na uhasama zimeondoka na wananchi kufanya shughuli zao za maendeleo,” alisema.
Masoud aliwataka wananchi kuendelea kutekeleza maridhiano hayo na kuyaenzi kuhakikisha yanakuwa endelevu kwa maslahi ya wananchi wa Zanzibar katika kupiga hatua ya maendeleo.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Ismail Jussa aliwataka wananchi kuiunga mkono ACTWazalendo kwani kipo kwa ajili ya kuleta maelewano na kuwaunganisha wananchi wote katika kukuza shughuli zao za kiuchumi na maendeleo.
Katika Kijiji cha Marumbi Wilaya ya Kati Unguja, Othman alizindua tawi la chama na kuwataka wanachama wake kukiunga mkono kuhakikisha kinashinda katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.