Napenda kuungana na mamilioni ya Watanzania kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Joseph Magufuli kwa uzalendo na mapenzi ya dhati anayoonyesha kivitendo kwa Wananchi na Taifa kwa ujumla kwa kuhakikisha analinda rasilimali, Mali, haki na maslahi.
Hivi karibuni Rais Magufuli alizuia makontena 277 yenye mchanga wa madini kusafirishwa kwenda nje ya nchi na kuunda kamati kuchunguza hasara au faida tuliyokuwa tukiipata Watanzania kutokana na kusafirisha mchanga huo ambapo kamati imewasilisha taarifa ya awali imeonyesha thamani ya makontena hayo 277 ni Tsh. Bilioni 112.1 kumbe thamani halisi ni Tsh. Trilioni 1.44. Taarifa hiyo imeonyesha hayo makontena tu tulikuwa tumepoteza zaidi ya Tsh. Bilioni 829.4 ambapo kwa mwaka mmoja tu tulikuwa tukipoteza Trilioni 25 ambayo Serikali ilikuwa haipati hata senti moja.
Kupitia mchanga huo tu tulikuwa tukiibiwa hivyo kwa takribani miaka 18 huku tukipoteza Tsh. Trilioni 829.4 sawa na bajeti ya miaka 26 ya Tsh Trilioni 32 kwa kila mwaka.
Tunapoteza pesa hizo huku tukiangalia mahospitali hayana madawa, miundombinu mibovu, mishahara haikidhi, tunakopa kukamilisha bajeti ya nchi maumivu ambayo hatukustahili kabisa kuyapata sisi Watanzania.
Ahsante sana Rais Magufuli kwa kuonyesha uzalendo wa kuzuia unyonyaji na uhujumu uchumi huu wa kikatili uliokuwa ukiendelea nchini. Ni viongozi wachache sana Afrika waliosalia wenye kariba ya uzalendo kama alionao Rais Magufuli.
Huu ni mwendelezo wa uzalendo wa kivitendo unaoonyesha na Rais Magufuli. Tukumbuke ni Rais Magufuli huyu huyu anasimamia vyema upotevu wa mapato bandarini, kuzuia matumizi ya ovyo Serikalini ya kodi za Wananchi kwa kufuta safari za nje, kulipana posho zisizo na tija na kupunguza matumizi ya kawaida kwa kuongeza fedha zaidi kwenye matumizi ya kimaendeleo.
Kiukweli ninaiona Tanzania mpya ikijengwa na uzalendo alionao Rais Magufuli kwa Watanzania na Taifa kwa ujumla. Watendaji, viongozi na Wananchi yatupasa tuige Uzalendo wa Rais wetu mpendwa Dk. John Pombe Magufuli kwa kuungana nae kupambana na wahujumu uchumi wa nchi yetu.
Rais Magufuli fanya uliyotumwa na wanyonge usiogope wanaojiita wachambuzi ambao kila kitu hukuchambua kinyume, hao ni changamoto ya wewe kusonga mbele!
Tunakuombea Rais Magufuli ulinzi, Baraka, hekima na busara zaidi toka kwa Mwenyezi Mungu.
Mungu Ibariki Tanzania
Mungu mbariki Rais wetu Dk. Magufuli.
Na Emmanuel J. Shilatu
25/05/2017
0767488622
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.