NA ALBERT G.SENGO/BUKOMBE/GEITA
Serikali kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) imeingia makubaliano ya ushirikiano na kampuni ya uchimbaji madini ya Plantcor ya Afrika Kusini kwa lengo la kufanya utafiti na baadaye uchimbaji wa madini katika Pori na Hifadhi ya Msitu wa Kigosi, wilayani Bukombe mkoani Geita. Makubaliano hayo yamesainiwa Jumanne, Februari 24, 2026 katika Ukumbi wa CCM Bukombe, hafla iliyohudhuriwa na Naibu Waziri wa Madini, Steven Kiruswa kama mgeni rasmi. Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Kiruswa amesisitiza umuhimu wa mwekezaji kuhakikisha kuwa zoezi la utafiti, litakalotumia teknolojia ya kisasa ya ndege nyuki (drones) kabla ya kuanza rasmi uchimbaji wa dhahabu, linafanyika kwa uwazi na kwa kutoa taarifa sahihi kwa wananchi ili waweze kushirikishwa na kunufaika na matokeo ya utafiti huo. Aidha, amemtaka mwekezaji huyo kuwekeza katika kuboresha miundombinu ya eneo husika, hususan barabara, kupitia mpango wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR), ili kurahisisha upatikanaji wa maeneo ya uchimbaji kwa wachimbaji wadogo. Ameeleza kuwa hali ya miundombinu ilivyo sasa hairidhishi na inahitaji maboresho ya haraka. Mradi huo unatarajiwa kuwa chachu ya uchumi katika wilaya hiyo kupitia kodi za mirabaha, uboreshaji wa miundombinu na huduma za kijamii kwa wananchi pamoja na ajira za muda mfupi na mrefu zipatazo 2,000.Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment