ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Thursday, February 26, 2026

BARABARA MLIMA KITONGA KUPANULIWA NA KUWA NJIA NNE

news

WAZIRI wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amesema serikali iko katika hatua za mwisho za kuanza upanuzi wa barabara inayopita Mlima Kitonga mkoani Iringa ambayo sasa itakuwa ya njia nne na yenye taa za barabarani.

Amesema hatua hiyo ni uamuzi wa Rais Samia Suluhu Hassan ili kupunguza foleni na kuboresha usalama wa watumiaji wa barabara katika njia hiyo inayotumiwa na magari mengi. 

Akizungumza jana baada ya kutembelea eneo hilo, Waziri Ulega, alisema barabara hiyo ni ya kimkakati kwa uchumi wa nchi kwa sababu inatumiwa pia na magari yanayokwenda katika nchi zinazotumia bandari ya Dar wa Salaam kubeba mizigo yao. 

Akitoa picha ya ongezeko la uhitaji wa upanuzi wa barabara hiyo, Waziri Ulega alisema idadi ya magari yanayopita katika Barabara Kuu ya TANZAM imeongezeka kutoka magari 1,700 hadi 3,400 kwa siku, hali inayosababisha njia hiyo kuzidiwa.

Waziri wa Ujenzi Abdala Ulega akizungumzia upanuzi wa barabara Mlima Kitonga.

“Nimepokea mapendekezo kutoka kwa Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Iringa ya kuhakikisha tunaondoa msongamano wa magari katika Mlima Kitonga, na nimeelekeza kwa wataalamu wetu kupanua hii barabara kwa kilometa saba. Kwa sasa hivi barabara ina njia mbili kwa hiyo tutatanua na kuwa njia nne,” alisema Ulega.

Waziri Ulega aliongeza kuwa ni maelekezo ya Rais Samia kwamba kila mradi wa barabara uende sambamba na uwekaji wa taa za barabarani ili kuhakikisha usalama wa watumiaji ikiwemo wananchi, wafanyabiashara na madereva pamoja na kuweka kingo pembezoni mwa barabara ili kuzuia magari yasianguke kwenye makorongo.

“Ninaagiza manunuzi yaanze mara moja ili kuhakikisha kwamba barabara hii inatanuliwa kwani ina umuhimu mkubwa katika uchumi wa nchi hivyo hatuwezi kuiacha katika hali hii na kutimiza pia maelekezo ya rais kutatua changamoto zote,” alisema Ulega. 

Mbunge wa Jimbo la Kilolo, Ritha Kabati, alisema barabara hiyo ni ya uchumi wa kimataifa hivyo ikitengenezwa itainua zaidi uchumi wa Mkoa wa Iringa na taifa kwa ujumla pamoja na kuwasaidia wananchi ambao hupata changamoto ya kufuata huduma za kijamii ikiwemo matibabu Iringa mjini. 

Meneja wa TANROADS Mkoa wa Iringa Eng. Yudas Msangi alisema gharama ya upanuzi wa kilometa saba kwa njia mbili katika barabara hiyo ni bilioni 59.2 na ukarabati wa njia mbili zilizopo ni bilioni 16.2.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment