ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Monday, July 15, 2024

UWT KIBAHA MJI YAFANYA KWELI YATEMBELEA MATAWI 14 KUHIMIZA ZOEZI LA KUJISAJILI

 


NA VICTOR MASANGU,KIBAHA 


Mwenyekiti wa Umoja wa wanawake Wilaya ya Kibaha mjini (UWT) Elina Mgonja  katika kuelekea katika uchaguzi wa serikali za mitaa amefanya ziara ya kikazi na kufanikiwa  kuyatembelea jumla ya  matawi 14  kwa lengo la kuweza  kujionea hali halisi ya uandikishaji kwa njia ya kieletroniki.

Ziara hiyo ambayo imefanyika katika kata mbili za Tangini na Maili moja pia ilikuwa na lengo la kuwahimiza wanawake kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi katika kushiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa.

Akizungumza katika ziara hiyo ya kikazi Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Kibaha mjini Elina Mgonja amesema kwamba ameamua kufanya ziara hiyo akiwa na wajumbe wa kamati ya utekelezaji ili kujionea mwenendo mzima wa zoezi la uandikishaji wa wanachama wa CCM  kwa njia ya kieletroniki.


Pia Mgonja alibainisha kwamba wamebaini kuwepo kwa mwamko mkubwa kwa wanawake kujitokeza kwa wingi katika zoezi hilo la kujisajili kwa njia ya kisasa kwa ajili ya kuweza kujiandaa na uchaguzi wa serikali za mitaa ambao unatarajjwa kufanyika mwaka huu.

"Mimi kama Mwenyekiti nimeambatana na wajumbe wa kamati ya UWT na tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutembelea matawi 14 ambayo yapo katika kata ya Tangini pamoja na kata ya maili moja na tumekuta idadi kubwa ya wanawake wamejisajili kwa mfumo wa kieletroniki,"alisema Mgonja.


Mgonja amesema kwamba lengo ni kuhakikisha wanakuwa na wanachama wengi wa CCM ambao wamesajiliwa kwa njia ya kisasa pamoja na kujiandikisha katika daktari la wapiga kura lengo ikiwa ni kufanya vizuri na kushinda kwa kishindo katika uchaguzi wa serikali za mitaa. 


Kadhalika Mgonja amewahimiza makundi mbali mbali ya wakinamama,vijana,wazee pamoja na wanachama wote kujiandikisha katika daftari la kupiga kura pamoja na kuboresha taarifa zao ili waweze kupata fursa ya kushiriki katika uchaguzi huo.

Katika hatua nyingine Mwenyekiti huyo amempongeza kwa dhati Rais wa awamu ya sita Dkt.Samia Suhuhu Hassan kwa kuweza kutoa fedha kwa ajiili ya utekelezaji wa miradi mbali mbali ya maendeleo  ikiwemo katika  sekta ya afya.maji,elimu,pamoja na miundombinu ya barabara. 


Mgonja amemshukuru kwa dhati Mbunge wa Jimbo la Kibaha mjini Silvestry Koka pamoja na mke wake Mama Selina Koka  kwa kuweza kushirikiana kwa hali na mali katika kuwasaidia wanawake katika suala zima la kuleta maendeleo chanya katika nyanja mbali mbali.

Kwa upande wake Katibu wa UWT Kibaha mjini Cecilia Ndaru amewahimiza wanachama kuweka misingi mizuri ya kupendana na kuwa na umoja hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguguzi wa serikali za mitaa.

 Katika ziara hiyo ya UWT Mwenyekiti huyo ameambatana na viongozi mbali mbali wa chama cha mapinduzi  wakiwemo baadhi ya madiwani wa kuchaguliwa pamoja na wale madiwani wengine wa viti maalumu sambamba na viongozi wengine wa UWT.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.