NA VICTOR MASANGU, KIBAHA
Umoja wa wanawake (UWT) Wilaya ya Kibaha mjini imewataka wanawake kuachana na tabia ya kufanya kampeni za chini chini kabla ya muda haujafika wa kampeni na badala yake wametakiwa kuwapa ushirikiano wa kutosha viongozi ambao wapo madarakani hadi kipindi cha muda wao utakapomalizika bila ubaguzi wowote.
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Umoja wa wanawake (UWT) Wilaya ya Kibaha mjini Selina Mgonja wakati akizungumza na baadhi ya wakinamama wa UWT kata za Kibaha pamoja na viziwaziwa ikiwa ni ziara yake ya kikazi yenye lengo la kuzungumza na wanachama sambamba na kuwahimiza wanawake wenye sifa na vigezo kushiriki na kujitokeza katika uchaguzi wa serikali za mitaa.
Mgonja alisema kwamba kwa sasa ni vema viongozi mbali mbali ambao walichaguliwa na wananchi na wapo madarakani kwa mujibu wa sheria wanatakiwa kuheshimiwa na kupewa ushirikiano wa kutosha katika suala zima la utekelezaji wa Ilani ya chama na sio kuanza kuwabeza na kuwaandaa watu mwingine kinyemela kabla ya muda wake kumalizika kwani amechaguliwa kihalali.
"Katika ziara yangu lengo kubwa ni kutembelea katika kata mbali mbali ambazo zipo katika Jimbo la Kibaha mjini na kuwahimiza wanawake wenzangu kuweza kujitokeza kwa wingi kuchukua fomu kwa ajili ya kugombea nafasi lakini kitu kikubwa wanatakiwa kuwaheshimu viongozi wa chama ambao bado wapo madarakani na kuachana na tabia ya kutengeneza safu ya uongozi kabla ya wakati,"alisema Mgonja.
Aidha Mwenyekiti Mgonja amebainisha kuwa lengo lingine la kufanya ziara hiyo ni kuwajengea uwezo wanawake ili wapate fursa ya kujiamini na kugombea katika uchaguzi wa serikali za mitaa bila ya kuwa na uwoga wowote na kwamba wana imani ziara hiyo itaweza kuleta mabadiliko chanya kwa wanawake kujitokeza kwa wingi.
Katika hatua nyingine aliwataka wanawake wa UWT kuendelea kumpa ushirikiano wa kutosha Rais wa awamu ya sita Dkt. Samia Suluhu Hassan kwani ameweza kutenga fedha nyingi ambazo zimetumika katika miradi mbali mbali ya kimaendeleo hivyo wanawake wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kumsemea yale mazuri ambayo ameyafanya katika kipindi cha miaka mita.
Kwa upande wake Katibu wa UWT Wilaya ya Kibaha mjini Cesilia Ndalu alisema kwamba katika kuelekea uchagzui wa serikali za mitaa wanawake wanapaswa kuwa na uthubutu na ujasiri kwa lengo la kuweza kujitosa kuchukua fomu na kushiriki katika uchaguzi huo ambao unatarajiwa kufanyika mwaka huu.
Nao baadhi ya wanawake wa UWT wamempongeza Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Kibaha mjini Elina Mgonja kwa ziara yake hiyo ya kikazi ambayo imeweza kuwapa hamasa zaidi katika kushiriki kugombea katika uchaguzi wa serikali za mitaa.
Naye Diwani wa viti maalumu Halmashauri ya mji Kibaha Selina Wilson amewakumbusha wanawake hao kutumia ujuzi na maarifa waliyonayo katika kuhakikisha wanakuwa mstari wa mbele katika kugombea nafasi za uwenyekiti katika uchaguzi wa serikali za mtaa mbao unatarajiwa kufanyika mwaka huu.
Ziara ya Mwenyekiti wa umoja wa Wanawake (UWT) Wilaya ya Kibaha mjini imelenga kupita katika kata zote 14 za Jimbo la Kibaha mjini ambapo kwa leo ziara imefanyika katika kata mbili za Kibaha pamoja na kata ya Viziwaziwa ambayo ni ya nane kufikiwa siku ya leo kwa lengo la kuwahimiza wanawake kujitokeza kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa serikali za mitaa.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.