ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Saturday, August 14, 2021

UCHAGUZI ZAMBIA:- HICHILEMA ACHUKUA UONGOZI WA MAPEMA DHIDI YA LUNGU.

 


Kiongoizi wa upinzani nchini Zambia Hakainde Hichilema amechukua ushindi wa mapema.

Matokeo ya awali yaliyotangazwa na tume ya uchaguzi yanaonesha chama cha National Development kinaongoza kwa idadi ya kura dhidi ya Rais Edgar Lungu.

Mwandishi wa BBC Nomsa Maseko anasema Raia wa Zambia wanasubiri kwa hamu kujua ni nani atakuwa rais wao mpya.

Tume ya uchaguzi imekuwa ikijumuisha kura zilizopigwa Alhamisi katika uchaguzi uliyokuwa na ushindani mkali.

Matokeo ya maeneo bunge 15 kati ya zaidi ya 150 yametangazwa kufikia sasa.

Matokeo katika maeneo bunge hayo ambayo yanatajwa kuwa ni ngome za Lungu, yanaashiria kuwa Hichilema amepata uungwaji mkono mkubwa katika ngome za mpinzani wake tofauti na uchaguzi wa mwaka 2016 uliogubikwa na madai wa wizi wa kura.

Uwepo mkubwa wa wanajeshi bado unaonekana katika barabarani huku ulinzi mkali ukiwekwa katika kituo cha kutangaza matokeo.

Baadhi ya wagombea urais wamekubali kushindwa na kumpongeza Hakainde Hichilema, kiongozi wa chama cha United Party for National Development kwa kuchukua ushindi wa mapema katika uchaguzi huo.

Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Patrick Nshindano, amewaambia waandishi habari mjini Lusaka kuwa jumla ya kura 296,210 zilipigwa katika maeneo bunge hayo.

Matokeo ya kwanza yaliyotarajiwa kutolea jana Ijumaa yalichelewa baada ya zoezi la kuhesabu kura kuendelea hadi usiku kutokana na idadi kubwa ya wapiga kura, na pia kwa sababu baadhi ya vyama vya kisiasa vilipinga matokeo yaliyotolewa na tume hiyo katika eneo bunge moja.

Kwengineko Mamlaka ya Mawasiliano na Teknolojia nchini Zambia imepelekwa mahakamani kwa kudhibiti huduma za intaneti na mitandao ya kijamii waziri wa Mamlaka tangu Alhamisi.

Mahakama kuu ya Zambia imeamuru marufuku hiyo kuondolewa mara moja.

CHANZO: BBC SWAHILI.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.