Ripoti ya jeshi la polisi nchini Tanzania inaonesha ongezeko la asilimia 25.95 la ukatili dhidi ya watoto. Katika mwaka 2020 visa 7388 viliripotiwa kote nchini tofauti na mwaka 2015 ambapo matukio 5,803 yaliripotiwa.
Watetezi wa masuala ya haki za watoto wametaja imani za kishirikina na utandawazi kuwa miongoni mwa sababu za kuongezeka kwa matukio hayo.
Ripoti hii ya Jeshi la Polisi inakuja katika kipindi hiki ambacho wazazi na walezi wengi wanatajwa kutokuwa karibu na watoto wao, wengi wakijihusisha na kusaka maisha bora ili kukidhi mahitaji ya msingi ya watoto huku wakiwapora haki ya kuwasikiliza.
Ripoti ya jeshi la polisi inataja miongoni mwa ukatili dhidi ya watoto ulioripotiwa kwa kiwango kikubwa kuwa dhuluma za kingono ambapo katika mwaka wa 2020 kuliripotiwa visa 7263 ikiwa ni ongezeko la asilimia 26 ikilinganishwa na mwaka 2015 ambapo vilirikodiwa visa 5803, hii ikiwa ni sawa na visa 615 kwa mwezi jambo ambalo linatajwa kuwa linahatarisha mustakabali wa ustawi kwa watoto nchini humo.
Takwimu hizo zinarandana vilivyo na zile zilizotolewa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu Tanzania, katika ripoti yake ya hali ya haki nchini humo mapema mwaka huu, ambayo ilionesha kuongezeka kwa kiwango cha kutisha kwa matukio ya aina hiyo dhidi ya watoto.
Wanaharakati: Imani za kishirikina zachangia ukatili dhidi ya watoto Tanzania
Anna Henga ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu Tanzania, amesema ongezeko hilo ni kutokana na kukithiri kwa imani za kishirikina miongoni mwa wanajamii wanaotaka kusaka utajiri huku maeneo yaliyomulikwa zaidi ni upande wa Kanda ya Ziwa,
Aidha, ripoti zote mbili zimekwenda mbele zaidi na kuonesha kwa mwaka 2020 kulikuwa pia na wasiwasi juu ya ukatili juu ya watoto unaofanywa na watoto wenyewe, hasa matukio ya watoto kulawitiana katika shule za msingi na sekondari, matukio ambayo vyombo vya habari vilihusika kuyaripoti kwa asilimia 87.
Utandamazi na mmomonyoko wa maadili walaumiwa
Sophia Temba Afisa Program Jukwaa la Utu wa Mtoto, Kitengo cha Ulinzi wa Mtoto. Amesema Mmomonyoko wa maadili na kutamalaki kwa utandawazi ndani ya jamii ni miongoni mwa sababu zinazoongeza kasi ya matukio hayo, lakini kuna haja ya kutengwa bajeti ya kutosha kutekeleza mpango kazi wa taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto, kunahitajika sasa.
Baadhi ya wazazi na walezi waliozungumza na JEMBE FM wanasema kwamba kuongezeka kwa rekodi ya matukio haya ni matokeo chanya, kwani ni kunatokana na kushamiri kwa elimu kwenye jamii ambapo hapo kabla yalitokea na watu waliyamaliza katika ngazi ya familia wakihofia sheria kuchukua mkondo wake, uhasama baina ya ndugu na visasi huku wakisahau afya za waathirika.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.