ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Wednesday, November 24, 2021

HOTUBA YA WAZIRI GWAJIMA KWENYE MKUTANO MKUU CHAMA CHA WATAALAMU WA USTAWI WA JAMII ULIOFANYIKA JIJINI MWANZA

 


HOTUBA YA MHESHIMIWA WAZIRI DR. DOROTHY GWAJIMA (MB), KATIKA KONGAMANO LA WATAALAMU NA WATOA HUDUMA ZA USTAWI WA JAMII KATIKA UKUMBI WA BENKI YA TANZANIA  (BOT) TAREHE 24-27, NOV 2021

 

·        Mhandisi Robert Gabriel: Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,

·        Dkt Nandera E. Mhando, Kamishna wa Idara ya Ustawi wa Jamii,

·        Dkt.  Mariana Makuu, Mwenyekiti wa TASWO:

·        Wawakilishi wa Mashirika na Wadau wa huduma za ustawi wa jamii:  UNICEF, ABBOT FUND, PACT, SOS VILLAGES

·        Viongozi wa TASWO,

·        Waadhiri wa vyuo vikuu vinavyozalisha Wataalamu wa Ustawi wa Jamii,

·        Maafisa Ustawi wa Jamii kutoka Mikoa ya Tanzania Bara,

·        Wadau na Watoa huduma za Ustawi wa Jamii,

·        Ndugu Wanahabari,

·        Wageni waalikwa,

·        Mabibi na Mabwana,

Nawasalimu kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania...

 

Awali ya yote napenda kuchukua nafasi hii kumshukuru Mwenyenzi Mungu mwingi wa rehema kwa kutujalia uhai, uzima na nafasi ya kujumuika pamoja katika kongamano la mwaka la Chama cha Wataalamu wa huduma za ustawi wa Jamii nchini. Pia, napenda kuwashukuru kwa kunialika kuwa mgeni rasmi katika kongamano hili. Aidha, nawapongeza kwa maandalizi mazuri mliyoyafanya kwa lengo la kufanikisha kongamano hili.  Kipekee niushukuru uongozi wa Mkoa wa Mwanza kwa kutoa ushirikiano na kuturuhusu kufanya shughuli hii katika Mkoa huu.

 

Naomba mtambue ya kwamba serikali kupitia Wizara yangu itaendelea kuimarisha mfumo wa utoaji huduma za ustawi wa jamii na kuhakikisha kwamba haki za watu wenye mahitaji maalumu walio pembezoni wanapata huduma zote za msingi kwa wakati.

 


Ndugu Wanataaluma ya Ustawi wa Jamii,

Natambua kwamba Chama cha Wataalamu wa Ustawi wa Jamii kimekuwa kikifanya kazi kwa karibu na serikali kwa kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) pamoja na wadau wengine wa maendeleo katika kutatua changamoto mbalimbali zinazokwamisha utoaji wa huduma bora za ustawi wajamii. Wizara yangu inatambua mchango mkubwa wa TASWO katika kusimamia na kutetea haki za wanataaluma, watoa huduma pamoja na makundi nufaika ya huduma za ustawi wa jamii hapa nchini.

 

Ndugu Wanataaaluma ya Ustawi wa Jamii,

Kauli Mbiu ya mwaka huu 2021 ni “UBUNTU”. Hili ni neno la Kizullu lenye maana ya “I AM because WE ARE”. Kauli mbiu hii ni nzuri kwani inasisitiza umuhimu wa umoja, ushirikiano na kusaidiana kwa lengo la kumuimarisha kila mtu na hivyo kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma za ustawi wa jamii. Zaidi, kauli mbiu hii inasaidia kukuza mahusiano baina yetu na kusaidia kuwaweka watoa huduma na wanufaika na huduma karibu hivyo kutoa fursa ya kujenga mshikamano kwa ajili ya kupanga namna ya kutafuta ufumbuzi wa matatizo yanayoikabilI jamii.

Kwa kusema haya nipende kusisitiza umuhimu wa kukuza na kusimamia mahusiano kati yetu kama watoa huduma na wanufaikaji wa huduma zinazotolewa.

Ndugu Wanataaluma ya Ustawi wa Jamii,

Nipende kuwapongeza Maafisa Ustawi wa Jamii katika ngazi zote za utoaji wa huduma kwa umahiri mkubwa wanaounyesha na kwa jitihada mnazochukua kushughulikia changamoto na matatizo mbalimbali ya masuala ya: migogoro ya ndoa na familia, huduma kwa wazee na watu wenye ulemavu, ukiukwaji wa haki za watoto pamoja na ukatili wa kijinsia.

 


Ndugu Wanataaluma ya Ustawi wa Jamii,

Ninatambua kuwa, Wataalamu wa Ustawi wa Jamii wanafanya kazi kubwa sana katika Idara ya Afya kupitia vituo vya afya, hospitali za wilaya , hospitali za mikoa pamoja na hospitali za rufaa. Maafisa hawa hutumika kutoa huduma za msaada wa kisaikolojia na ushauri nasaha kabla na baada ya matibabu, maelekezo ya namna ya kujikinga na maambukizi zaidi ya magonjwa, kushiriki kampeni za elimu kwa umma, ufuatiliaji na tafiti za kijamii kwa lengo la kutoa huduma bora za afya kwa wahitaji, utambuzi na usimamizi wa huduma za msamaha kwa wagonjwa na wazee. Pamoja na hayo, maafisa hawa wanahamasisha jamii, kufanya utambuzi na kuwaunganisha wanajamii na Wazee katika Bima ya Mfuko wa Afya Jamii (CHF).

 

Ndugu Wanataaluma ya Ustawi wa Jamii,

Pamoja na kazi nzuri mnazozifanya kwa makundi yote maalumu hapa nchini, ninatambua kuwa, bado kuna changamoto mbalimbali ndani ya jamii zetu ikiwemo ongezeko la watoto wa mitaani ambalo limekuwa likiongezeka siku hadi siku. Hadi sasa kuna jumla ya watoto wanaoishi na kufanyakazi mitaani ni 5,390 (1,538 wasichana na 3,852 wavulana) walitambuliwa katika Mikoa ya Mwanza, Arusha, Iringa, Mbeya and Dodoma. Kati ya watoto hao, jumla ya Watoto 135 (43 Ke and 92 Me) waliweza kuunganishwa na familia zao, watoto 821 (302 Ke and 519 Me) waliweza kupewa vifaa saidizi na kupelekwa shuleni, na watoto 75 (17 Ke and 58 Me) walipewa mafunzo ya uanagenzi.

 

Ndugu Wanataaluma ya Ustawi wa Jamii,

Ongezeko la watoto wa mitaani limechangiwa na mambo mbalimbali yanayojitokeza katika jamii kama vile: kutengana kwa wazazi, wazazi kujikita zaidi katika utafutaji maisha na uzalishaji mali, umasikini wa kaya, vifo vya wazazi na walezi, msukumo wa makundi rika kutokana na mmomonyoko wa maadili katika jamii na wakati mwingine hulka ya mtoto mwenyewe.

 


Ndugu Wanataaluma ya Ustawi wa Jamii,

Wizara yangu inaendelea kutekeleza jukumu la ulinzi na usalama wa Watoto walio katika mazingira hatarishi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali. Kipekee nipende kuushukuru Mfuko wa ABBOT kwa kuweza kuunga mkono jitihada za serikali, ambapo kwa pamoja tumeweza kufanikisha ujenzi wa Makao ya Taifa ya Watoto Kikombo yaliyoko katika jiji la Dodoma. Makao ya Taifa ya Watoto Kikombo, yalizinduliwa rasmi tarehe 16 Juni, 2021 na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dr. Philip Isdory Mapango. 

 

Ndugu Wanataaluma ya Ustawi wa Jamii,

Makao ya Taifa ya Watoto Kikombo, yana uwezo wa kuhudumia watoto 250, hivi sasa kuna jumla ya Watoto 55, kati yao wakiume ni 34 na wakike ni 21. Makao hayo yana nyumba za kuishi watumishi, kituo cha huduma za ufundi na uanagenzi pamoja na kituo cha kulelea watoto wadogo mchana.

Huduma za msingi zinazotolewa katika makao hayo kwa ajili ya Watoto ni pamoja na huduma za afya, elimu, chakula, malazi na mavazi. Pamoja na hayo watoto hao hupatiwa huduma ya mafunzo ya uanagenzi, ushauri nasaha na msaada wa kisaikolojia ikiwa ni pamoja na kuwaandaa kuwaunganisha na jamii na familia zao.

 

Ndugu Wanataaluma ya Ustawi wa Jamii,

Wizara yangu inaendelea kutoa huduma kwa watoto walio katika mkinzano na sheria katika shule ya Maadilisho Irambo. Kwa kipindi cha miaka mitano, kuanzia 2017-2021, shule hiyo imeweza kuwahudumia watoto 154 (148 Me na 06 Ke). Katika mwaka huu wa fedha 2020/2021 kuna jumla ya Watoto 36 (33 Me na 3 Ke) wanaoendelea kupatiwa huduma ya marekebisho ya tabia, unasihi, uanagenzi na kuunganishwa na jamii baada ya kumaliza kutumikia adhabu zao.  Aidha, Serikali inaendelea kusimamia mahabusu za Watoto tano (5) zinazotoa huduma ambazo ziko katika Mkoa wa Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Mbeya na Dar es Salaam na tupo katika hatua za mwisho za marekebisho ya Mahabusu ya Watoto Mtwara. Kwa muda wa miaka mitano iliyopita kuanzia 2017-2021 kuna jumla ya Watoto 315 (277 Me na 38 Ke) wameweza kupatiwa huduma katika Mahabusu hizo za Watoto nchini.

 

Ndugu Wanataaluma ya Ustawi wa Jamii,

Kwa mwaka wa fedha 2020/2021 Wizara iliweza kupokea jumla ya maombi 149 ya malezi ya kambo na kuasili. Miongoni mwa maombi hayo, maombi 50 yalipatiwa vibali vya kuendelea na mchakato wa malezi ya kambo, ambapo watoto 38 (20 Ke na 18 Me) walipatiwa ya malezi ridhaa ya malezi ya kambo na Watoto 17 (12 Ke na 5 Me) waliasiliwa.

 

Aidha, Wizara imeweza kusajili jumla ya vituo 301 vya kulelea Watoto Wadodo mchana vilivyosajiliwa na Vituo 33 vya kulelea Watoto Wachanga viliweza kupata usajili. Idadi hiyo inapelekea kuwa na jumla ya Vituo vya kulelea watoto wadogo mchana 1,844 kwa nchi nzima. Katika vituo vya kulelea Watoto Wadodo mchana vilivyosajiliwa kuna jumla ya Watoto 163,394 (85,175 Me na 78,219 Ke).

 

Vilevile, tunaendelea na usajili wa Makao ya Watoto yanayotoa huduma kwa Watoto walio katika mazingira hatarishi, hadi sasa kuna jumla ya  Makao 239 nchi nzima.

 

Ndugu Wanataaaluma ya Ustawi wa Jamii,

Wizara imekamilisha kufanya mapitio ya Sera ya Wazee ya mwaka 2003 na kuandaa andiko la Sera hiyo, Mpango wa Utekelezaji wake na Waraka wa wasilisho la Sera katika Baraza la Mawaziri ambalo tayari limeshawasilishwa. Serikali imeendelea kufanya utambuzi wa kaya masikini na kutoa bima za afya na matibabu bila malipo kwa wazee na jamii kwa ujumla. Jitihada hizo zimefanyika tangu mwaka 2015 ambapo hadi kufikia Juni, 2021 jumla Wazee wasiojiweza 2,203,414 (1,198,338 Ke na 1,005,076 Me) walitambuliwa. Jumla ya Wazee 1,256,544 wameweza kupatiwa kadi za bima ya Afya na matibabu bila malipo.

Hadi kufikia sasa kuna jumla ya madirisha ya huduma kwa Wazee 2,335 katika hospitali na vituo vya afya kwa ajili ya kuharakisha na kutoa huduma za afya stahiki kwa Wazee nchi nzima.

 


Ndugu Wanataaaluma ya Ustawi wa Jamii,

Tumeendelea na utoaji huduma ya makazi kwa wazee wasiojiweza hapa nchini kwa kushirikiana na wadau. Hivi sasa tuna jumla ya makazi ya Wazee 15, ambayo yana jumla ya Wazee 291, kati yao Wanaume ni 180 na Wanawake ni 111. Huduma katika makazi hayo hutolewa na serikali kwa kushirikiana na wadau wa huduma kwa wazee.

Aidha, wizara imeendelea kuratibu na kusimamia huduma katika makazi binafsi ya Wazee hapa nchini, ambapo hivi sasa kuna jumla ya makazi binafsi ya Wazee 14 yanayotoa huduma kwa Wazee 451, kati yao Wazee 216 ni wanaume na 235 ni wanawake.

 

Ndugu Wanataaaluma ya Ustawi wa Jamii,

Hata hivyo, tunaendelea kuenzi makubaliano mbalimbali ya kitaifa ikiwa ni pamoja na siku ya Wazee dunia ambayo huadhimishwa kila ifikapo tarehe 01 Oktoba ya kila mwaka. Kwa mwaka 2020/2021 kwa kushirikiana na Mkoa wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Wizara iliweza kushiriki katika maadhimisho hayo yaliyofanyika katika Wilaya ya Kondoa, ambapo jumla ya Wazee 226 kutoka katika Halmashauri 8 za Mkoa wa Dodoma na wengine kutoka Dar es Salaam waliweza kushiriki kilele cha siku hiyo. Katika siku hiyo, jumla ya Wazee 111 walipatiwa huduma bila malipo ya uchunguzi wa Afya na tiba.

 

Wizara yangu kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI, imeweza kushiriki katika utatuzi wa migogoro ya ndoa na familia. Jumla ya migogoro 4,932 iliweza kushigulikiwa. Nitumie fursa hii kuahidi kuendeleza ushirikiano na wataalamu wa ustawi wa jamii kwa ujumla wao katika kuhakikisha huduma za ustawi wa jamii zinaboreshwa na zinawafikia walengwa kwa wakati. Niwapongeze wadau wote ambao wameendelea kushirikiana na serikali za kijamii nyakati zote. Mnekuwa bega kwa benga na serikali katika kutoa misaada ya kibinadamu na huduma ya kisaikolojia kwa wananchi hasa kipindi hiki ambacho nchi inapitia janga la UVIKO-19.

 

Ndugu Wanataaaluma na watoa huduma za ustawi wa Jamii,

Wizara inatumbua kuwa, sekta ya ustawi wa jamii ni mtambuka kwa maana ya huduma zake zinatakiwa kila sehemu kama vile idara ya afya kwa kiwango kikubwa sana, mashuleni, wizara mbalimbali, halmashauri zote kwa kiwango kikubwa kuanzia Mkoa, Wilaya, Kata na Vijiji, Idara na Taasisi mbalimbali, nk. Hii imepelekea kuwe na uhitaji mkubwa sana wa wataalam kwa kiwango ambacho serikali haiwezi kumudu kuajili mara moja. Hivyo, naagiza, wakati Serikali inaendelea kujipanga kuona namna ambayo itaongeza kuwaajiri wataalamu hawa, basi idara mbalimbali zitumie mwongozo wa Wizara wa kuajiri wataalamu wakujitolea ili kupunguza uhaba huo. Nitoe wito kwa wadau wote kutumia mwongozo wa kitaifa wa watu wanaojitolea kusaidia kuajiri wataalam wa ustawi wa jamii katika ngazi mbalimbali ili kukidhi utoaji wa huduma.

 


Ndugu Wanataaaluma ya Ustawi wa Jamii,

Ninatambua uwepo wa changamoto mbalimbali zinazokwamisha utoaji wa huduma bora na zenye viwango kwa wanajamii katika ngazi ya msingi, ambapo miongoni mwa changamoto hizo ni:

§  Ufinyu wa bajeti katika Sehemu / Kitengo cha Ustawi wa Jamii chenye dhamana ya kuzifikia jamii na utekelezaji wa afua mbalimbali zinazolenga kutoa suluhu ya matatizo ndani ya jamii,

§  Muundo wa Idara ya Ustawi wa Jamii na namna unavyochangia kukwamisha utoaji wa huduma bora na taarifa za utendaji. Hivi sasa eneo la huduma kwa Watu wenye Ulemavu lipo katika Ofisi ya Waziri Mkuu, wakati Sehemu ya Huduma za Familia, Watoto, Watoto walio katika Mkinzano na Sheria pamoja na Wazee wapo chini ya Wizara ya Afya, maendeleo ya Jamii, Jinsia, na Wazee,

§  Muungano dhaifu wa kimawasiliano na kitendaji kati ya Idara ya Ustawi wa Jamii na Sehemu ya Ustawi wa Jamii katika Ofisi ya Rais – TAMISEMI unasababisha kukwama kwa uratibu madhubuti wa utoaji huduma na kupelekea ukosefu wa taarifa na takwimu sahihi za kitendaji kutokana na utekelezaji wa afua za huduma za ustawi wa jamii. Tatizo hili lilipata kuwepo upande wa Idara za Afya za pande zote mbili ila kwa sasa limepungua sana,

§  Uhaba wa Maafisa Ustawi wa Jamii katika Halmashauri za Wilaya.

Ndugu Wanataaaluma ya Ustawi wa Jamii

Serikali imechukua hatua mbalimbali kwa lengo la kuboresha utoaji huduma za ustawi wa jamii ikiwa ni pamoja na kutoa miongozo ya huduma na kuratibu mafunzo kwa maafisa Ustawi wa Jamii waliopo katika Halmshauri mbalimbali hapa nchini. Zoezi hilo ni endelevu na linatekelezwa na serikali kwa kushirikiana na wadau wa huduma za Ustawi wa Jamii hapa nchini.

 

Ndugu Wanataaluma ya Ustawi wa Jamii,

Nimesikia risala iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa TASWO Taifa kuhusiana na changamoto mbalimbali zinazokwamisha huduma za ustawi wa jamii kutolewa kwa ubora unaotakiwa. Serikali imeendelea kuzifanyia kazi baadhi ya changamoto hizo.

 

Ndugu Wanataaluma ya Ustawi wa Jamii,

Wizara yangu kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI na ufadhili kutoka Shirika la PACT TANZANIA, UNICEF na JSI tumefanikiwa kutoa Mwongozo wa Mipango na Bajeti ya Huduma za Ustawi wa Jamii katika ngazi ya Halmashauri (Comprehensive Council Social Welfare Operational Guideline - CCSWOPG) unaolenga,

§  kuweka uwiano sawa maeneo ya vipaumbele vya huduma za ustawi wa jamii kwa nchi nzima,

§  kuweka uwiano wa afua za utatuzi wa changamoto katika jamii,

§  kuwa na uhakika wa huduma kwa wakati kwa makundi yote yaliyo katika mazingira hatarishi,

§  kuweka uwanda mpana wa wadau kuunda afua jumuishi za utatuzi wa changamoto katika jamii,

§  kuboresha na kuimarisha ushirikiano baina ya wadau na watoa huduma za ustawi wa jamii,

§  Kuweka uchambuzi sanifu wa mahitaji ya huduma za kijamii, kubaini rasilimali zilizopo na aina ya huduma inayopaswa kutolewa.

Ndugu Wanataaluma ya Ustawi wa Jamii,

Ninajua mna kiu na hamu kubwa ya kuona sheria ya Taaluma ya Ustawi wa Jamii inakamilika na kuanza kutumika ili iweze kuweka udhibiti kwa wanataaluma na watoa huduma za ustawi wa jamii. Sheria hiyo itaweka bayana viwango vya ubora wa huduma vinayotakiwa katika jamii.  Aidha, itakuwa msingi mzuri wa uanzishaji wa baraza la usimamizi na udhibiti wa wanataaluma na watoa huduma za ustawi wa jamii nchini.

Wizara yangu inatambua umuhimu sheria hiyo, hivyo napenda kuwahakikishia kuwa tupo katika hatua za mwisho za ukamilishaji wake, na mara itakapokamilika nitaiwasilisha katika mamlaka husika ili iweze kupata ridhaa ya kuanza kutumika ndani ya nchi yetu.

 

Ndugu Wanataaluma ya Ustawi wa Jamii,

Ni kweli kuna uhaba wa Maafisa Ustawi wa Jamii, hata hivyo, Wizara  imeendelea kuomba vibali vya ajira kwa ajili ya kupunguza tatizo lililopo na kufika huduma stahiki kwa wanajamii. Hivyo, kadiri tutakavyopatiwa watumishi wapya, wizara yangu itawapangia kazi katika maeneo na vituo vyenye uhitaji zaidi kwa lengo la kuboresha huduma.

Suala la Muungano dhaifu wa kimawasiliano na kitendaji kati ya Idara ya Ustawi wa Jamii na Sehemu ya Ustawi wa Jamii katika OR-TAMISEMI limeshatafutiwa ufumbuzi ambapo kuanzia mwezi Septemba, 2021 kumekuwa na vikao vya kiutendaji baina ya pande hizi mbili vinavyolenga kushirikishana mipango na mikakati madhubuti ya utaoji huduma jumuishi katika jamii. Vikao hivi vitakuwa vinafanyika kwenye kila robo ya mwaka wa fedha kuanzia mwaka huu wa fedha 2021/2022.

 Changoto ya muundo wa Idara kati ya Wizara Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, na Ofisi ya Waziri Mkuu nimelipokea na niahidi kuliwasilisha katika mamlaka husika. 

 

Ndugu Wanataaaluma ya Ustawi wa Jamii,

Ninawasihi muendelee kuelimisha jamii kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa UVIKO-19 kwa kuvaa barakoa, kutumia vitakasa mikono, kunawa mikono kwa maji tiririka na kutokukusanyika sehemu moja bila sababu ya msingi. Aidha, nitoe rai kwa jamii waendelee kupata chanjo ya UVIKO-19 inayotolewa katika vituo vya Afya na hospitali maalumu nchi nzima. Aidha, ninawaomba muanze kutoa elimu kwa umma ili wananchi waweze kujiandaa kushiriki Sensa ya Watu na Makazi inayotarajiwa kufanyika mwaka 2022 kwa nchi nzima.

 

Mwisho.

Ninawapongeza sana Maafisa Ustawi wa nchi nzima kwa kutekeleza maazimio mbalimbali ya Kimataifa, Kikanda pamoja na Miongozo, Sera na Sheria za nchi zinazotolenga kutoa huduma bora na ulinzi kwa makundi yote maalumu mnayoyahudumia.

Baada ya kusema hayo, sasa natamka rasmi kuwa, kongamano la Wataalamu na watoa huduma za ustawi wa jamii limefunguliwa rasmi.

 

NAWASHUKURU KWA KUNISIKILIZA NA NAWATAKIA KONGAMANO JEMA

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.