ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Thursday, September 18, 2025

MASHAHIDI 100 KUWASILISHA USHAHIDI KESI YA KUPOROMOKA JENGO KARIAKOO

Mashahidi 100 kuwasilisha ushahidi kesi ya kuporomoka jengo Kariakoo

Zaidi ya mashahidi 100 wanatarajiwa kuwasilisha ushahidi katika kesi ya mauaji bila kukusudia inayowakabili wafanyabiashara sita, kufuatia kuporomoka kwa jengo la ghorofa mnamo Novemba 16, 2024, katika Mtaa wa Mchikichi na Kongo, Kariakoo jijini Dar es Salaam.

Kesi hiyo iliwasilishwa leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa ajili ya kusomwa maelezo ya mashahidi na vielelezo kwa washitakiwa. Hata hivyo, hatua hiyo haikufanyika kutokana na upande wa mashtaka kutokamilisha maandalizi.

Wakili wa Serikali, Clemence Kato, aliieleza mahakama kuwa kesi hiyo inatarajiwa kuwa na mashahidi zaidi ya 100, lakini hadi sasa ni nusu pekee ya mashahidi ambao maelezo yao yamekwishachapwa.

“Waheshimiwa, tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kusoma maelezo ya mashahidi na vielelezo kwa washitakiwa, kwa kuwa bado hatujakamilisha maandalizi,” alisema Wakili Kato mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geofrey Mhini.

Baada ya kusikiliza hoja hizo, Hakimu Mhini alikubaliana na ombi la upande wa mashtaka na kuahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 9, 2025.

Washitakiwa:-

Wafanyabiashara wanaokabiliwa na kesi hiyo ni:

  • Lendela Mdete, mkazi wa Mbezi
  • Zenabu Islam maarufu kama Zaibanu, mkazi wa Kariakoo
  • Ashour Ashour, mkazi wa Ilala
  • Soster Nziku na Stephen Nziku, wakazi wa Mbezi Beach
  • Aloyce Sangawe, mkazi wa Sinza Wanadaiwa kusababisha vifo kwa uzembe baada ya jengo walilohusishwa nalo kuporomoka na kuua wakazi na wafanyakazi waliokuwemo.

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka, jalada hilo bado halijakamilika na linasubiri kuwasilishwa katika Mahakama Kuu, kutokana na uzito wa kosa linalowakabili washitakiwa.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment