ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Thursday, May 1, 2025

PADRI KITIMA AVAMIWA NA KUJERUHIWA POLISI YAMSHIKILIA MTU MMOJA.

 


Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linachunguza tukio la kushambuliwa kwa Padri Charles Kitima, Katibu wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), ambaye alijeruhiwa kichwani usiku wa kuamkia Mei Mosi, 2025 katika eneo la maliwato ya kantini ya TEC, Kurasini.


Kwa mujibu wa taarifa ya Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, tukio hilo lilitokea majira ya saa nne na robo usiku.


Padri Kitima alikuwa ametoka kuhudhuria kikao cha viongozi wa dini kilichodumu kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa moja jioni. Baada ya kikao hicho, aliendelea kubaki katika kantini ya Baraza kwa ajili ya kupata kinywaji, ambapo baadaye alielekea maliwatoni na ndipo alipovamiwa na kushambuliwa na watu wawili waliotumia kitu butu.


Padri Kitima alipelekwa katika Hospitali ya Aga Khan kwa ajili ya matibabu na hali yake inaelezwa kuwa inaendelea vizuri. Kabla ya kuhamishiwa Aga Khan, alipatiwa huduma ya kwanza katika kituo kidogo cha afya kilichopo ndani ya eneo la TEC.


Jeshi la Polisi linamshikilia mtu mmoja, Rauli Mahabi (maarufu kama Haraja), mkazi wa Kurasini, kwa ajili ya mahojiano kuhusiana na tukio hilo huku uchunguzi wa kina ukiendelea ili kuwabaini wote waliohusika na kuhakikisha hatua kali zinachukuliwa mara moja.


Mashuhuda waliokuwepo katika eneo la tukio wameripoti kuwa Padri Kitima alionekana akizungumza na watu kadhaa kabla ya kuondoka kuelekea maliwatoni, na muda mfupi baadaye waliona watu wakikimbia eneo hilo, huku yeye akiomba msaada akiwa anatokwa damu.


Padri Charles Kitima mbali na kuwa Katibu wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), mbali na nafasi yake ndani ya Kanisa Katoliki, Padri Kitima anajulikana kwa misimamo yae ya kukosoa na kuwa mstari wa mbele katika masuala ya haki za binadamu, utawala wa sheria na uwajibikaji wa kijamii.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.