
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara limemkamata Ibrahimu Nzumbi Mugendi (31), mkazi wa Kijiji cha Makere, Wilaya ya Kasulu, kwa tuhuma za kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Kwa mujibu wa taarifa ya polisi, mtuhumiwa aliwasili mkoani Mtwara Februari 18, 2026 na kufikia katika nyumba ya kulala wageni (jina limehifadhiwa). Februari 26, 2026 alifika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mtwara kupitia Ofisi ya Katibu Tawala wa Wilaya, ambapo aliomba kibali cha kukusanya michango kutoka kwa watu binafsi na taasisi mbalimbali akidai kuwa ana changamoto ya kuongea (bubu).
Alifanikiwa kupatiwa kibali hicho chenye kumbukumbu namba B58/274/03/123, na kuanza kuzunguka katika taasisi za serikali pamoja na kwa watu binafsi akiomba michango.
Hata hivyo, baada ya uchunguzi wa kina, ilibainika kuwa mtuhumiwa hana tatizo lolote la ulemavu wa kuongea, bali alitumia kigezo hicho kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Mtuhumiwa alikamatwa katika nyumba hiyo ya kulala wageni akiwa na kiasi cha Shilingi 1,800,000 alizokuwa amechangiwa na taasisi pamoja na watu binafsi ndani ya Wilaya ya Mtwara.
Uchunguzi wa awali umeonesha kuwa alifanikiwa kufika katika jumla ya taasisi 10 za serikali na binafsi. Polisi wamesema upelelezi unaendelea, na ukikamilika mtuhumiwa atafikishwa kwenye vyombo vya sheria kwa hatua zaidi.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment