
TAKRIBANI wananchi 169,638 wa Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara wamekumbwa na mafuriko makubwa yaliyosababisha uharibifu wa makazi, mali na mashamba, hali inayozidi kuongeza ugumu wa maisha kwa wakazi wa eneo hilo.
Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Fakii Lulandala, amesema licha ya idadi hiyo ya wananchi walioathirika lakini pia mafuriko hayo yameharibu zaidi ya ekari 97,429 za mashamba kwa kujaa maji.
Imeelezwa kuwa mafuriko hayo yameathiri kwa kiasi kikubwa kata za Shambalai, Nduruma, Mirerani na Naisinyai, ambako maji yameingia ndani ya nyumba na kusomba mali mbalimbali pamoja na kuharibu vyanzo vya chakula, huku ukihitajika msaada wa dharura.
“Athari hizo zimeacha wananchi wengi bila makazi, chakula na mahitaji muhimu, na wengine wamelazimika kuishi kwa ndugu na jamaa wakati wakisubiri msaada zaidi,” amesema.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi, mkazi wa Mererani, Henson Loy, amesema tatizo la mafuriko limekuwepo kwa muda mrefu lakini mwaka huu limeongezeka kwa kiwango kikubwa zaidi.
“Moja ya sababu kuu ya hali hiyo ni miundombinu mibovu ya mifereji ya maji pamoja na barabara kuwa chini, hali inayosababisha maji kushindwa kupita na hivyo kuelekezwa moja kwa moja kwenye makazi ya wananchi,” amesema.Mkazi wa Utupendana, Jonathan Mkali, amesema mafuriko hayo hujitokeza mara kwa mara kila msimu wa mvua na hudumu kwa muda mrefu, hali inayosababisha usumbufu mkubwa kwa wananchi ikiwemo kukatika kwa mawasiliano na shughuli za kiuchumi.
Katika juhudi za kusaidia waathirika, kampuni ya Permanent Minerals imetoa msaada wa vifaa mbalimbali ikiwemo chakula vifaa vya shule vya watoto,vyandarua,venye thamani ya takriban Sh. milioni 22, ikiwa ni sehemu ya mchango wa wadau katika kukabiliana na athari za mafuriko hayo.
Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya ameendelea kutoa wito kwa taasisi mbalimbali, mashirika na wananchi kujitokeza kusaidia zaidi, akisisitiza kuwa mahitaji bado ni makubwa kutokana na ukubwa wa janga hilo.
Aidha, wananchi wameiomba serikali kuchukua hatua za kudumu kwa kuboresha miundombinu ya mifereji ya maji, kupanua mitaro na kuinua barabara ili kuzuia kujirudia kwa mafuriko hayo katika siku zijazo.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment