ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Friday, April 3, 2026

POLISI MWANZA YASISITIZA MARUFUKU DISKO TOTO

news 

JESHI la Polisi Mkoa wa Mwanza limesisitiza marufuku ya kuandaa burudani za watoto katika kumbi za starehe (disko toto) likisema marufuku hiyo inalenga kulinda rika hilo na vitendo vya uvunjifu wa amani na kupotea.

Marufuku hiyo imesisitizwa leo Aprili 3, 2026 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa, wakati akizungumzia maandalizi ya kuimarisha ulinzi na usalama kuelekea sikukuu hizo.

Pia Mutafungwa amepiga marufuku wazazi kuwaruhusu watoto kwenda kwenye matembezi ama sehemu za burudani bila uangalizi wa watu wazima, huku akisisitiza kila mzazi kuhakikisha anaangalia watoto ili washerehekee wakiwa na ulinzi wa kutosha.

“Niwatake wamiliki wa nyumba za kulala wageni na kumbi za starehe kuendesha shughuli zao kwa kuzingatia masharti ya leseni zao kwa kutoendesha na kuandaa matamasha ya watoto (disko toto) na kuhakikisha maeneo hayo yamewekewa ulinzi wa kutosha.

“Na tunaelekeza kwa namna yoyote mambo ya kuburudisha watoto disko toto mambo hayo ni marufuku na hatutasita kuchukua hatua za sheria kwa wafanyabiashara watakaofanya hivyo hata kama wana leseni, na tunaomba wazazi wasiwaruhusi kwenda huko,” amesema Mutafungwa.

Hata hivyo, ametoa wito kwa familia zinazosherehekea sikukuu nje ya makazi yao kutoacha nyumba zao zikiwa hazina uangalizi wowote.


“Wanapotoka wahakikishe nyumba ina ulinzi. Pia tunashauri wasitoke wote ndani ya nyumba, wabaki baadhi ya watu wanaoangalia nyumba ili kuepuka kupata changamoto,” amesema.

Amesema jeshi hilo limeimarisha ulinzi maeneo yote kwa kuwapanga askari wanaotumia doria za magari, pikipiki, magari ya wazi, askari wa kiraia, askari wanaotumia wanyama, na limeshaweka mpango kazi wa doria za boti katika visiwa vinavyozungika mkoa huo.

“Tunaomba kila mwananchi awe na utii mkubwa wa sheria na kuepuka mambo ambayo yanaweza kuwaweka kwenye migogoro na vyombo ambavyo vinasimamia sheria,” amesema Mutafungwa.

Vile vile, amewataka viongozi wa makanisa yatakayokuwa na ibada za asubuhi na usiku kuendelea kushirikiana na polisi katika ngazi ya wilaya na vituo ili kuhakikisha katika ibada zote askari wanakuwepo.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment