WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamo wa Rais (Muungano na Mazingira), Hamad Yusuf Masauni, amesema serikali inatarajia kufanya maboresho ya sheria ili kuipa mamlaka zaidi Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kushughulikia moja kwa moja wanaokiuka sheria za mazingira, bila kujali kama ni taasisi za umma au binafsi.
Akizungumza Machi 30, 2026 katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha usimamizi wa taka ili kulinda mazingira na afya za wananchi.
Aidha, Masauni amewataka wananchi kutumia kilele cha maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Taka Sifuri kama fursa ya kujifunza namna ya kubadilisha taka kuwa rasilimali yenye tija, hatua itakayosaidia kuongeza kipato na kukuza uchumi wa taifa.
Ameongeza kuwa NEMC inahitaji kupatiwa vitendea kazi vya kisasa, ikiwemo helikopta na droni, ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yake na kudhibiti uchafuzi wa mazingira.
Sambamba na hilo, ametoa onyo kali kwa wote wanaochafua mazingira, wakiwemo wazalishaji wa mifuko ya plastiki, wanaotupa taka hovyo, wanaomwaga maji machafu baharini na wanaosababisha kelele mitaani, akisisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa bila upendeleo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amesema mkoa wa Dar es Salaam umeanza mpango wa kufundisha somo la uhifadhi wa mazingira kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, ambapo tayari shule 10 zimechaguliwa kuanza utekelezaji wake.
Tupe maoni yako





0 comments:
Post a Comment