Watawa kutoka mkoani Arusha, wakikabidhiwa cheti cha Ushindi wa Afya Mazingira jijini Dodoma, na Waziri wa Afya Dkt. Dorothy Gwajima wakati wa siku ya Mwisho ya Mkutano wa Maafisa Afya nchini uliomalizika mkoani Dodoma
Na Atley Kuni, WAMJW, DODOMA
Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Dorothy Gwajima, amesema, Chanjo, Lishe na Afya Mazingira ni maeneo muhimu ambayo yanabeba sehemu kubwa ya sekta ya Afya kwa ujumla wake na endapo wakifanikiwa kwenye maeneo hayo basi yatatokea mapinduzi makubwa katika Sekta ya Afya.
Dkt. Gwajima, amesema hayo leo Desemba 17, 2021 wakati akifunga Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Maafisa Afya Mazingira uliomalizika Jijini Dodoma kwa siku tatu ukihusisha Maafisa Afya na Wadau mbalimbali wa ajenda ya Afya Mazingira kutoka kwenye Mikoa yote 26 nchini, Halmashauri 184.
Dkt. Gwajima amesema, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan inatoa kipaumbele cha kutosha kwenye eneo hili kwani inatambua kuwa ni eneo muhimu katika kuboresha afya za watanzania. Na kwa kuzingatia umuhimu mwaka wa fedha 2019/2020 serikali imetoa kiasi Shs.25, 628, 654,250 kwa ajili ya utekelezaji wa programu endelevu ya maji na usafi wa mazingira na mwaka 2021/2022 imetoa Sh.28,467,204,790 kwa ajili hiyo ambapo zimetumika kujenga miundombinu ya maji, vyoo na vichomea taka katika vituo 660 vya kutolea huduma za afya nchini.
Dkt. Gwajima amewapongeza Maafisa Afya kwa kazi nzuri wanayoendelea kufanya tangu kuzinduliwa kwa zoezi la uchanjaji wa Chanjo ya UVIKO 19 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan. Amesema, Maafisa Afya Mazingira wameendelea kutekeleza jukumu husika kikamilifu kwa kutoa elimu ya afya na kuwezesha jamii kubadilika kifikra juu ya upotoshaji uliokuwa ukiendelea juu ya chanjo.
“Pamoja na kupata chanjo, tunahitaji pia kuimarisha kinga ya miili yetu kwa kupata lishe bora inayotokana na kula mlo kamili ikiambatana na mazoezi ya mwili ambayo ni msingi wa afya njema. Ili wananchi waendelee kupata chakula bora na salama, Maafisa Afya Mazingira mna jukumu kubwa la kusimamia hili kwa kuhakikisha ubora na usalama wa chakula unazingatiwa hasa katika maeneo yote yanayouza bidhaa za chakula na vinywaji,” amesema Dkt. Gwajima.
Dkt. Gwajima amesema tafiti zinaonesha kwamba, sehemu kubwa ya matatizo ya kiafya yanayoshughulika nayo ni yale ambayo yanaweza kuzuilika kwa njia ya usafi wa mazingira huku wakitolea mfano kuwa, wastani wa wagonjwa sita (6) wa nje (OPD) kati ya kumi (10) wanaohudhuria katika vituo vya kutolea huduma za Afya wengi wao wanasumbuliwa na magonjwa ambayo yanaweza kudhibitiwa kwa njia ya usafi wa mwili na mazingira. Hivyo, kwa namna yeyote ile lazima eneo hili liimarishwe ili kuleta tija ndani ya sekta.
Mkutano huo ambao ulikuwa umebebwa na kaulimbiu ya Imarisha Huduma za Afya Mazingira na Usafi katika Mapambano ya UVIKO-19, Dkt. Gwajima amesema, inaakisi manufaa mtambuka kwa Afya Mazingira katika kukabiliana na kuenea kwa ugonjwa wa UVIKO-19. Ameongeza kwa kusema, Afya Mazingira ni eneo pana linalojumuisha matumizi ya vyoo bora; usalama wa chakula; usalama wa maji ya kunywa; udhibiti wa taka ngumu; udhibiti wa majitaka; udhibiti wa uchafuzi wa hewa; udhibiti wa wadudu wadhurifu; makazi bora; usafi wa mwili; udhibiti wa magonjwa yanayoenezwa Kimataifa; utupaji wa mabaki ya binadamu; udhibiti wa kemikali na afya mahali pakazi.
Katika Hafla hiyo Mhe. Gwajima ameitaja Mikoa Vinara kwa Usafi wa Mazingia kwa Mwaka 2021 kuwa ni Manyara iliyopata asilimia 97.6, ukifuatiwa na Katavi ulipata asilimia 82.9 na Mkoa wa tatu ni Dodoma ulipata asilimia 80.5. Dkt. Gwajima amekabidhi vyeti na tuzo mbalimbali kwa washindi. Aidha, kwa niaba ya seriakli ameahidi kuhakikisha kunakuwa na vikao vya kuongeza kasi ya ufuatiliaji wa utekelezaji kwa njia ya mtandao kila baada ya miezi mitatu na kwa cha kwanza ni tarehe 30 Januari, 2021.
Awali akitoa taarifa rais wa Chama cha Maafisa Afya Mazingira Tanzania Twaha Mubarak ameishukuru Serikali na Wadau wa Maendeleo ambapo kupitia Taasisi ya Benjamini Mkapa kwa mwaka 2020/21 imewezesha ajira ya 171 za wataalamu wa afya mazingira na kupunguza uhaba kwa asilimia mbili.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.