Na WAMJW, Dodoma
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ameihakikishia Dunia kusimamia eneo la Haki ya Usawa wa kiuchumi kwa wanawake Tanzania ikiwa ni eneo la pili kati ya maeneo Sita ya kizazi chenye usawa.
Mhe. Rais Samia ameyasema hayo wakati akizindua Kamati ya Kitaifa itakayoshauri nchi kuhusu utekelezaji wa ahadi za nchi kwenye Jukwaa la kizazi chenye usawa leo tarehe 16 Desemba, 2021 jijini Dodoma.
Rais Samia amesema sehemu kubwa ya Dunia haijatoa nafasi ya kutumia asilimia 50 ya nguvu kazi ya Wanawake katika kuimarisha Maendeleo ya uchumi.
Ameongeza kuwa wanawake bado ni waathirika wakubwa katika mabadiliko na athari za kiuchumi na kisiasa yanayoendelea katika maeneo mbalimbali na tafiti zinaonesha nguvu kazi hiyo ikitumika vizuri itachangia Dola za Kimarekani trilioni 28.
Amesema, ni muda sasa wa kuzifanyia kazi kikamilifu sera, sheria na mipango inayowekwa na Serikali ya kuinua Hali ya uchumi ya kuleta ustawi wa jamii na Taifa kwa ujumla ili kuweza kufikia malengo hivyo ni lazima kuwe na usimamizi, uratibu utathmini na ufuatiliaji wa sera na utekelezaji wa mipango.
"Baada ya miaka 20 tangu kutolewa kwa azimio la Beijing la kumkomboa mwanamke bado Serikali nyingi zimeshindwa kutekeleza sera ya kumuinua mwanamke kutokana vikwazo mbalimbali ikiwemo Afya, elimu, Mila kandamizi, mitaji, masoko, teknolojia na unyanyasaji wa aina mbalimbali" amesema Rais Samia.
Aidha, amebainisha kuwa Serikali imeridhia na inatekeleza mikataba na maazimio ya kikanda na Kimataifa ikiwemo mkataba wa kutokomeza aina zote za ubaguzi Kwa wanawake wa mwaka 1978, azimio la Bejing la mwaka 1995 na mkataba wa Kimataifa wa haki za mtoto wa 1979.
Awali, akitoa taarifa ya Kamati hiyo Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima alisema kuzinduliwa kwa Kamati hii kutasaidia kuimarisha na kuharakisha kasi ya shughuli zilizopangwa katika kutekeleza ahadi zilizotolewa kufikia kizazi chenye usawa.
Dkt. Gwajima amesema umuhimu wa eneo hili la Haki na usawa wa kiuchumi kwa wanawake ni mkubwa katika kuendeleza jitihada za Serikali amabyo imedhamiria kwa dhati kuleta usawa wa kijinsia ambao ni msingi muhimu katika kuchochea Maendeleo ya Ustawi wa Jamii.
"Jukwaa limeainisha maeneo sita ya utekelezaji ambayo yanakabili changamoto za Wanawake, ukatili wa kijinsia, haki na usawa wa kiuchumi, haki za uzazi, mabadiliko ya tabianchi, Teknolojia na ubunifu na uongozi" amesema Mhe. Gwajima
Naye Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt . John Jingu, alisema uzinduzi huu ni kuashiria cha nchi kutekeleza kwa vitendo ahadi alizozitoa Mhe. Rais kupitia Makamu wa Rais Dkt. Phillip Mpango katika Jukwaa la usawa wa kijinsia lililofanyika mwezi Juni mwaka huu Jijini Paris.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.