ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Friday, December 17, 2021

MBARAWA 'AVURUGWA' MRADI WA BIL 11/-

 


Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, amemtaka mhandisi wa Jengo la abiria katika Uwanja wa ndege wa Mwanza kufika mara moja kurekebisha dosari katika mradi huo wa Sh bilioni 11 ambao ujenzi wake haujakidhi viwango vya kimataifa.


Vilevile ameita Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini (TAA), kushirikiana na wataalamu kushauri namna gani ifanyike ili ujenzi ukidhi viwango vinavyotakiwa.


Prof. Mbarawa amesema hayo jijini Mwanza wakati alipofika kukagua ujenzi wajengo hilo unaoendelea ambao mpaka sasa umefikia asilimia 85.


Amesema hajaridhishwa na mradi huo ambapo amesisitiza kuwa mradi huo umekosa vigezo vya kimataifa vinavyosimamiwa na Shirika la Kimataifa la Anga (ICAO).


“Mwenye dhamana ya viwanja vya ndege sio Mkoa wala Halmashauri bali ni TAA, nashangaa kusikia hakuna mhandisi anayesimamia jengo hili kutoka kwao hivyo basi naagiza watoke Dar es Salaam waje kusimamia hili jengo ili tupate thamani ya fedha na viwango vinavyostahili, hatutaki kufanya makosa alafu badae tuje tulaumiane”, amesema Prof. Mbarawa.


Ameongeza kuwa majengo yanayostahili kujengwa katika viwanja vya ndege vya kimataifa ni tofauti na majengo mengine kwani yana viwango vyake vinavyostahili ambapo hapa havikufatwa.


“Tunatakiwa kujenga jengo liatakalodumu miaka 20 hadi 30 hatuwezi kujenga hivi hivi tu hapa tulipofikia wataalam waje waangalie nini kiboreshwe ili jengo likidhi mahitaji”, amesisitiza Prof. Mbarawa.


Aidha, Prof. Mbarawa ameeleza kuwa Serikali inaendelea kuboresha viwanjavingi vya ndege hapa nchini na hiki Kiwanja cha Ndege cha Mwanza kinatarajiwa kuwa cha Kimataifa hivyo lazima fedha zinazotolewa thamani yake ionekane na kupitishwa kwa viwango vya Shirika la Kimataifa la Anga (ICAO).


“Sisi kama Serikali tutahakikisha fedha zinaletwa ila mwisho wa siku tunahitaji kuona thamani ya fedha na kila anayehusika asimame kwenye eneo lake”, amesema Prof. Mbarawa.


Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel, ameeleza kuwa Mkoa imekwishaunda timu ya watalaam na tayari wameshaleta specification, michoro sahihi na kazi zinanedelea za kuboresha jengo hilo ili likidhi viwango vinavyostahili.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.