Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia Afya, Dkt. Grace Magembe, akifungua Mkutano wa Mwaka wa Maafisa Afya jijini Dodoma
Baadhi ya Maafisa Afya wakiwa wanamsikiliza Dkt. Grace Magembe, Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI, wakati wa hafla ya Ufungzi wa Mkutano wa Maafisa hao wa Mwaka.
Anyitike Mwakitalima, Mkuu wa kitengo cha Chakula, Maji na Usafi wa Mazingira... Wizara ya Afya, akiongea wakati wa mkutano huo wa Mwaka
Mkurugenzi Msaidizi Kitengo cha Afya Mazingira na Usafi, Wizara ya Afya Dkt. Khalid Mansa, akitoa tathmini ya utekelezaji wa miaka minne kwenye masuala ya Afya Mazngira
Na Atley Kuni, WAMJW-DODOMA
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia Afya, Dkt. Grace Magembe, amewataka Maafisa Afya mazingira, kote nchini kuondoa woga katika utekelezaji wa majukumu yao na badala yake, wasimamie sheria wanapotekeleza wajibu wao.
Magembe amesema, Suala la Utunzaji wa Mazingira ndio msingi wa Afya Bora kwa wananchi na ndio inasaidia jamii kuondokana na magonjwa mbalimbali ikiwepo kipindupindu ambacho chanzo chake kikuu ni ulaji wa kinyesi.
Dkt. Magembe ametoa kauli hiyo mapema leo Desemba 15, 2021 wakati akifungua Mkutano wa Mwaka wa Maafisa Afya Mazingira unaondelea jijini Dodoma ambao umeratibiwa na Wizara ya Afya kwa ushirikiano na Ofisi ya Rais TAMISEMI pamoja na Wadau wa Maendeleo.
“Hamtakiwi kuwa wanyonge mnapotekeleza wajibu wenu, mimi nikiwa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, niliwahi kumng’ang’ania mtu aliyetupa uchafu kupitia dirisha la gari na alipo kaidi nilisimama kwenye msingi wa sheria hadi akapokea adhabu inayo mstahiki, hivyo lazima mjue dhamana mliyopewa ni kubwa ni vema mkaitendea haki”. Amesema Dkt. Magembe.
Awali akitoa taarifa ya Utekelezaji wa Masuala ya mazingira nchini, Mkurugenzi Msaidizi Kitengo cha Afya Mazingira na Usafi, Wizara ya Afya Dkt. Khalid Massa, amesema, kwa sasa hali ya watu kuwa na vyoo bora nchini imeongezeka kutoka asilimia 42 ya mwaka 2017 na kufikia asilimia asilimia 70 kwa mwaka 2021.
Dkt. Massa amesema mafanikio hayo yametokana na mikakati waliojiwekea hivyo kupunguza kaya zisizo kuwa na vyoo kutoka asilimia 9.6 hadi kufikia asilimia 1.3 kwa mwaka 2021.
Vilevile amesema vyombo vya kunawia mikono kwenye kaya vimeongezeka kutoka asilimia 5.6 ya mwaka 2017 hadi kufikia asilimia 41.7 kwa mwaka 2021, lakini pia wameendelea kuchukua hatua za kulinda mipaka kwa kuwaajiri na kuwapeleka vijana wapatao 70 kwa ajili ya masuala ya Afya Mazingira mipakani.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Maafisa Afya na Mazingira nchini Twaha Mubarak ameiomba Serikali, kuangalia utaratibu wa uteuzi wa Maafisa Afya hao, kwani kwa kipindi cha sasa hawaridhishwi na uteuzi wao kunafanywa na Mganga Mkuu wa Wilaya au wa Mkoa suala ambalo Dkt. Grace Magembe, aliyekuwa Mgeni rasmi katika hafla hiyo ameahidi kulifanyia kazi.
Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Maafisa Afya Mazingira wenye Kaulimbiu isemayo Uimarishaji wa huduma za Afya Mazingira na usafi katika mapambano ya Uviko -19 unafanyika jijini Dodoma, ukiwa na lengo la kujitathmini juu ya utendaji kazi wao na kuweka mikakati kwa ajili ya Mwaka ujao.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.