ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Friday, December 17, 2021

MKURUGENZI SHIRIKA LA KIVULINI APONGEZA MAONO YA RAIS SAMIA.

 

Rais wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza kwenye uzinduzi wa Kamati ya Ushauri ya Kitaifa itakayoshughulikia Utekelezaji wa Ahadi za Nchi kwenye Jukwaa la Kizazi chenye Usawa.

Mkurugenzi wa Shirika la Kutetea Haki za Wanawake na Watoto KIVULINI la jijini Mwanza, ndugu Yassin Ally amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa maono yake makubwa ya kufikiria kuanzisha Wizara mpya itakayoshughulikia masuala ya jinsia, maendeleo ya jamii na wanawake tofauti na ilivyo sasa ambapo masuala hayo yanashughulikiwa na Wizara moja ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Mkurugenzi huyo ametoa pongezi hizo Disemba 16, 2021 baada ya Rais Samia kuhitimisha hotuba yake aliyoitoa kwenye hafla ya uzinduzi wa Kamati ya Ushauri ya Kitaifa itakayoshughulikia Utekelezaji wa Ahadi za Nchi kwenye Jukwaa la Kizazi chenye Usawa iliyofanyika ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.
Mkurugenzi Mtendaji Shirika la KIVULINI, Yassin Ally.

Ndugu Ally amesema uamuzi wa Rais Samia una manufaa makubwa ikiwa ni pamoja na kuipunguzia mzito Wizara ya Afya na kuiongezea ufanisi kwenye utekelezaji wa majukumu yake huku pia ukiongeza ufanisi kwenye Wizara mpya itakayoshughulikia jinsia, maendeleo ya jamii na wanawake katika kusimamia Mipango, Sera na Bajeti.

Aidha ameongeza kuwa hatua hiyo pia itaimarisha Wizara hiyo mpya kuzisimamia vyema Halmashauri nchini ili kutenga bajeji kwa ajili ya utekelezaji wa mpango kazi wa kitaifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto (MTAKUWWA) pamoja na kuimarisha ushirikiano baina ya wadau wa maendeleo ya jamii, jinsia, wazee, wanawake na watoto.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Awali Rais Samia amesema uamuzi wake wa kuitenga Wizara ya Afya na Wizara itakayoshughulikia masuala ya jinsia, maendeleo na wanawake unalenga kuimarisha utekelezaji wa Sera na mipango ya Nchi huku pia ukiiondolea mzigo mzito Wizara ya Afya katika kupambana na majanga mbalimbali na kuboresha huduma za afya.

Amesema Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa pamoja zinafanya kazi kubwa na nzuri na jitihada bado zinaendelea kufanyika ili kuhakikisha kuwa yale yote yaliyoahidiwa yanatekelezwa vyema.
Wananchi na Viongozi mbalimbali waliohudhuria uzinduzi wa Kamati ya Ushauri ya Kitaifa itakayoshughulikia Utekelezaji wa Ahadi za Nchi kwenye Jukwaa la Kizazi chenye Usawa. 

Hata hivyo Rais Samia amesema licha ya kazi nzuri pamoja na jitihada zinazofanywa na Wizara hizo bado malengo yaliyokusudiwa hayajafikiwa vyema hivyo maamuzi yake ni kuitenga Wizara ya Afya na Wizara nyingine itakayoshughulikia masuala ya Jinsia, Maendeleo na Wanawake katika Serikali ya Muungano wa Tanzania na kwamba atamshawishi pia Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi ili naye afanye mabadiliko kama hayo.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.