ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Tuesday, December 14, 2021

WIZARA YA AFYA NCHINI TANZANIA YAANZISHA MFUMO WA KUPOKEA MAONI KUBORESHA HUDUMA

 


Na.WAMJW....DODOMA 14/12/2021

Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt Dorothy Gwajima ameanzisha utekelezaji wa mfumo wa kukusanya maoni toka kwa watendaji wa taasisi anazosimamia kuanzia makao makuu ya wizara idara zote mbili ya afya na maendeleo ya jamii. Mfumo huu una lengo la kuwa na utaratibu wa ndani wa watendaji kutoa maoni dhidi ya mifumo ya uendeshaji wa taasisi zao ili kuboresha kwa uendelevu mpango mkakati wa kuimarisha mifumo ya uendeshaji wa Taasisi anazosimamia kwa ajili ya kuongeza ufanisi katika utendaji kazi wa watumishi wa sekta hiyo.


Amebainisha hayo leo Tarehe 14 Desemba 2021 Jijini Dodoma katika ofisi za Wizara ya Afya jengo la Bima ya Afya na baadaye Mji wa Serikali Mtumba wakati akiendesha zoezi hilo la kikao maalumu cha Mtumishi Sema na Waziri wa Afya kwa Maoni na Maboresho Mahala pa Kazi. Akirejea hotuba yake aliporiti kama Waziri kwenye sekta hiyo Disemba, 2020 amesema ni kipindi cha mwaka mmoja sasa umepita hivyo ni sahihi kabisa kufanya tathmini rasmi na kusimika mfumo wa tathmini endelevu kwa ajili ya kuinua zaidi viwango vya ufanisi wa sekta.


Dkt. Gwajima amesema kuwa zikiwa zimebaki siku chache kukamilisha mwaka 2021 ameona vema kufanya tathmini hii ili kujipanga vema zaidi kwa kutumia uzoefu wa mwaka mmoja wa utekelezaji kwa lengo la kwenda kasi zaidi na kufikia matarajio ya wananchi kama ambavyo Mheshimiwa Rais anatarajia. Amesema, taasisi imara inajengwa kwa kujipima na kujitathmini kisha kuja na mpango wa pamoja ulioshirikishi katika wajibikaji wa pamoja uliojengwa kwenye mifumo imara zaidi iliyoshirikisha maoni na mtazamo wa pamoja. 


Dkt. Gwajima amesema Taasisi ya Afya inatakiwa kuwa kimbilio kwa wananchi wanaofika kupata huduma kwa kufanya kazi kwa bidii kujituma na kujitolea ili kuepuka changamoto mbalimbali ambazo hutokea kwa kukosa mifumo imara ya uendeshaji …." Ndugu watumishi hatua ya kwanza ya safari ya kwenda kwenye mfumo imara wa uwajibikaji wa pamoja inaanza na fikra ya pamoja kwamba ninalotamani mimi au sisi litokee liwe la wote. Amesema tusitake wateja tu ndiyo wafanye tathmini dhidi yetu bali hata sisi tufanyiane tathmini sisi kwa sisi kwa hoja na kwa nia njema ya kuboresha mifumo ya kiutendaji." Amesema Dkt Gwajima


Amesema kuwa tusioneane aibu katika utoaji wa maoni kwa kuwa hakuna aliye mkamilifu hata kama ni kiongozi wa ngazi ya juu anatakiwa kupata mrejesho na ushauri ili kuendelea kuboresha mifumo kwani sifa moja ya uongozi bora ni pamoja na ukweli, uwazi na ushirikishaji. hivyo watumishi wanatakiwa kuwa huru katika utoaji wa maoni kwani yatalindwa na kuthaminiwa na kufanyia kazi na mrejesho kutolewa na huu ndiyo utakuwa utaratibu wa maisha yetu mahala pa kazi (institutional culture). Watumishi wote kwa umoja wao waitikia wito huo ambapo, wametoa maoni yao kwa uhuru na kumkabidhi waziri wa afya.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu amemshukuru Mhe. Waziri kwa utaratibu huo ambao amesema ni nadra katika taasisi kwa viongozi kupimana…"Ni jambo la kihistoria kuwa na utaratibu huu kwani utasaidia kuwajenga watumishi wote kuwa na mtazamo mmoja kuanzia ngazi ya uongozi, mara nyingi viongozi huwa hawafahamu hali halisi ya changamoto za watumishi wa chini yao" amesema Dkt. Jingu.

Naye Mganga Mkuu wa Serikali Dkt Sichalwe amemshukuru  Waziri wa Afya Dkt. Gwajima kwa ubunifu aliouanzisha, huku akiwataka Watumishi waliojitokeza kuitumia fursa hiyo kama sehemu ya maboresho ili kuongeza ufanisi katika kuwahudumia wananchi.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.