Picha na maktaba.
MSIMAMIZI wa Uchaguzi Jimbo la Mbarali, mkoani Mbeya, Missana Kwangura amemtangaza Furaha Chalamila kuwa diwani mteule wa Kata ya Ipwani baada ya kupita bila kupingwa kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Akitangaza matokeo hayo, Kwangura alisema Chalamila amepita bila kupingwa baada ya wagombea wenzake waliochukua fomu kujitoa kwenye uchaguzi huo.
Alisema waliochukua fomu za kugombea walikuwa wanne kutoka vyama vya CCM, CCK, UDP na ACT-Wazalendo na kwamba vyama viwili vilirejesha fomu ambavyo ni CCM na ACT-Wazalendo. Alisema Novemba 16, mwaka huu, mgombea wa ACT-Wazalendo alijitoa na alikwenda kuapa mahakamani.
“Sheria ya Uchaguzi kifungu cha 45 kidogo cha 2 kinasema kwamba, endapo mgombea atabaki mmoja katika kata, Msimamizi wa Uchaguzi atakubaliana na hali hiyo na atatoa taarifa kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi pamoja na kumjulisha mgombea kwa barua kuwa amechaguliwa, ila atatakiwa kutangazwa siku ambayo uchaguzi mdogo unafanyika kwa mujibu wa ratiba,” alisema.
Baada ya kukabidhiwa hati ya ushindi, Chalamila aliahidi kuwawakilisha vyema wananchi wa Kata ya Ipwani kwenye Baraza la Madiwani la halmashauri ya wilaya hiyo.
“Nakishukuru chama changu cha CCM kwa kuniamini, hawakukosea kunichagua, nitafanyakazi na nyinyi bega kwa bega kupitia sera na Ilani ya CCM kutatua changamoto zilizopo zikiwamo za barabara, maji, afya, umeme na ninawaahidi sitawaangusha,” alisema Chalamila. Katibu wa CCM Wilaya ya Mbarali, Clemence Mponzi alieleza kufarijika chama hicho kupata diwani mwingine katika halmashauri hiyo.
Alimtaka diwani huyo mteule avunje makundi na ashirikiane na wenzake waliokuwa kwenye kinyang’anyiro. Chalamila amechukua nafasi hiyo kutokana na aliyekuwa diwani wa kata hiyo, Mahamud Banichuma Mlwale kufariki dunia Agosti 28, mwaka huu.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.