MABINGWA watetezi, Yanga SC wameibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya wenyeji, Azam FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara leo Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Chachu ya ushindi wa Yanga ni leo mshambuliaji wa zamani wa Azam FC, Mzimbabwe Prince Dube Mpumelelo aliyetoa pasi ya bao la kwanza lililofungwa na kiungo Muivory Coast, Peodoh Pacome Zouzoua dakika ya 11, kabla ya yeye mwenyewe kufunga la pili dakika ya 34 akimalizia pasi ya kiungo Mudathir Yahya Abbas.
Bao pekee la Azam FC limefungwa na beki Lusajo Elukaga Mwaikenda dakika ya 81 akimalizia mpira wa adhabu uliopigwa na kiungo Feisal Salum Abdallah kutoka upande wa kulia wa Uwanja karibu kabisa na eneo la kupigia kona.
Kwa ushindi huo, Yanga SC inafikisha pointi 67 katika mchezo wa 25 na kuendelea kuongoza Ligi Kuu kwa pointi 10 zaidi ya Simba SC ambao hata hivyo wana mechi tatu mkononi.
Kwa upande wao Azam FC baada ya kupoteza mchezo huo wanabaki na pointi zao 51 katika nafasi ya tatu wakiizidi pointi moja Singida Black Stars baada ya timu zote kucheza mechi 26.
COASTAL UNION YAICHARAZA SINGIDA BLACK STARS 2-1 MKWAKWANI
WENYEJI, Coastal Union wameibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Singida Black Stars katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Mkwakwani Jijini Tanga.
Mabao ya Coastal Union yamefungwa na viungo Josaphat Arthur Bada raia wa Ivory Coast aliyejifunga dakika ya 47 na Bakari Suleiman Msimu dakika ya 82, wakati bao pekee la Singida Bock Stars limefungwa na mshambuliaji Mghana, Jonathan Sowah kwa penalti dakika ya 76.
Kwa ushindi huo, Coastal Union inafikisha pointi 28 na kupanda kwa nafasi ya tatu hadi ya 10, wakati Singida Black Stars inabaki na pointi zake 50 nafasi ya nne baada ya timu zote kucheza mechi 26.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.