Naibu Katibu Mkuu wa
Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali akizungumza na Waandishi wa Habari wakati
alipotembelea Kampuni ya Uhifadhi Mafuta (TIPER) iliyopo jijini Dar-esalaam tarehe 31 Julai, 2021 kujionea hali halisi ya
uendeshaji wa kampuni hiyo.
Naibu Katibu Mkuu
Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni
ya Uhifadhi Mafuta (TIPER) Michael Mjinja wakati alipotembelea Kampuni hiyo
iliyopo jijini Dar-esalaam tarehe 31 Julai, 2021 kujionea hali halisi ya
uendeshaji wa kampuni hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Uhifadhi Mafuta (TIPER) Michael Mjinja akitoa maelezo kuhusu utendaji wa Kampuni ya TIPER kufuatia ziara ya Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali kwenye kampuni hiyo tarehe 31 Julai, 2021.
Na Dorina G. Makaya – Dar-es-salaam
Serikali imeiagiza
Kampuni ya Uhifadhi Mafuta (TIPER) kuhakikisha inatoa taarifa za uendeshaji wa
kampuni hiyo kwa wakati, ili kuepusha changamoto ambazo zinaweza kujitokeza
baadaye kutokana na kutokutoa taarifa kwa wakati.
Agizo hilo limetolewa
jijini Dar-esalaam tarehe 31 Julai, 2021 na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya
Nishati Kheri Mahimbali wakati wa ziara yake kwenye kampuni hiyo iliyolenga
kujionea hali halisi ya uendeshaji wa kampuni ya TIPER.
Katika ziara yake,
Naibu Katibu Mkuu Mahimbali, ametembelea kwenye maeneo mbalimbali ya kampuni
hiyo ikiwa ni pamoja na matenki ya kuhifadhia mafuta jambo ambalo ameonyesha
kuridhishwa na utendaji kazi wa kampuni hiyo.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji
wa Kampuni ya Uhifadhi Mafuta (TIPER) Michael Mjinja, ameishukuru Serikali kwa
kufika katika eneo hilo ambapo wameweza kukubaliana masuala mbalimbali ikiwa ni
pamoja na kupeana taarifa kwa wakati.
Amesema, licha ya mafanikio
waliyonayo, bado kuna changamoto zinazowakabili huku kubwa ikiwa kuharibika kwa
vifaa vya kusukuma mafuta pindi wanapoyatoa kwenye meli, vifaa ambavyo
havipatikani nchini hadi viagizwe nje ya nchi.
Kufuatia hali hiyo,
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali amesema, endapo taarifa
hizo zitatolewa mapema, itakuwa mwarobaini wa changamoto hizo.
Ziara hiyo ni mwanzo
wa ziara nyingine katika taasisi zote zenye ubia na Serikali katika Sekta ndogo
ya Mafuta hapa nchini kwa lengo la kuboresha ufanisi na utendaji.
Katika ziara hiyo,
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Kheri Mahimbali, aliambatana na baadhi
ya viongozi na wataalam kutoka Wizara ya Nishati, Shirika la Maendeleo ya Petroli
Tanzania (TPDC), Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA), Mamlaka ya
Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji Nchini Tanzania (EWURA) na Kampuni ya
Serikali ya Uagizaji na Usambazaji wa Mafuta nchini (TANOIL).
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.