NA ALBERT G. SENGO, MWANZA Kuelekea mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya Pamba Jiji na Young Africans (Yanga SC) utakaopigwa katika dimba la CCM Kirumba jijini Mwanza, Kocha Mkuu wa Yanga, Pedro Goncalves, amesema timu yake inatarajia upinzani mkali kutoka kwa wenyeji hao. Goncalves ameeleza kuwa Pamba Jiji ni timu imara inapocheza nyumbani, ikiwa bado haijapoteza mchezo wowote katika uwanja wake, huku timu kadhaa kubwa zikishindwa kuondoka na alama tatu hali inayoashiria ugumu wa mchezo huo. “Tunatarajia mazingira magumu ya mchezo. Uwanja hautaruhusu soka la kuvutia, lakini hilo halibadilishi malengo yetu. Tunapaswa kuwa imara, makini na kupambana ili kupata alama tatu,” amesema kocha huyo. Ameongeza kuwa wapinzani wao wanacheza kwa nguvu na kasi, wakitumia vyema faida ya uwanja wa nyumbani pamoja na sapoti kubwa kutoka kwa mashabiki wao. “Ni timu inayocheza kwa msukumo mkubwa wa mashabiki wake. Wanajua namna ya kutumia mazingira yao kwa faida yao, hivyo nasi tumelazimika kujiandaa kisaikolojia na kimkakati kukabiliana na hali hiyo,” aliongeza. Kocha huyo ameonyesha imani kubwa kwa kikosi chake, akisisitiza kuwa wachezaji wake wamekuwa wakionyesha ari, nidhamu na uwezo wa kujiboresha kila siku. “Nina imani kubwa na wachezaji wangu. Kesho tunahitaji kuonyesha moyo wa upambanaji, ushindani, nidhamu na umoja ili kufanikisha malengo yetu,” amesema. Kwa upande wake, beki wa Yanga, Israel Mwenda, aliyewakilisha wachezaji, amesema wanatambua umuhimu wa mchezo huo pamoja na ubora wa mpinzani wao. “Kwa niaba ya wachezaji wenzangu, tunatambua umuhimu wa mchezo wa kesho. Utakuwa na ushindani mkubwa na kila mmoja wetu analitambua hilo. Tumerejea katika ari ya ushindi na tunakusudia kuendeleza mwenendo huo,” amesema Mwenda. Aidha, ametoa wito kwa mashabiki wa Mwanza na maeneo ya jirani kujitokeza kwa wingi kuisapoti timu hiyo. “Tunawaalika Wananchi kujitokeza kwa wingi kutupa sapoti. Tunawahakikishia kuwa tutapambana kwa nguvu zote ili waondoke wakiwa na furaha,” aliongeza. Akijibu swali la waandishi wa habari kuhusu presha ya mchezo huo, Mwenda amesema hawana presha yoyote, akisisitiza kuwa kucheza katika klabu kubwa kama Yanga kunahitaji uzoefu wa kukabiliana na mazingira yoyote. “Hatuna presha. Unapocheza Yanga lazima uwe tayari kukabiliana na hali yoyote. Tumejielekeza katika maandalizi sahihi na umakini mkubwa tukitambua umuhimu wa mchezo huu,” alihitimisha.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment