![]() |
| Mwanafunzi huyo (aliyefunikwa uso) akiondolewa Katika Hospitali ya Wilaya ya Ukerewe na ofisa wa jeshi la polisi dawati la jinsia. |
Katika tukio la kushangaza na lisilo la kawaida, mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Colnel Magembe iliyopo Wilaya ya Ukerewe, Mkoa wa Mwanza (jina limehifadhiwa), amepatikana akiwa hai baada ya kudaiwa kushambuliwa na kuchukuliwa na mamba takribani wiki moja iliyopita.
Tukio la kutoweka kwa mwanafunzi huyo lilitokea Machi 2, 2026 katika kitongoji cha Ilondo Magharibi, kijiji cha Buzegwe, Kata ya Kagunguli wilayani Ukerewe. Inadaiwa kuwa saa 11 alfajiri alipokuwa akioga katika Ziwa Victoria akijiandaa kwenda shuleni, alishambuliwa na mamba na kubebwa majini.
Hata hivyo, jana Jumatatu Machi 9, 2026, majira ya saa 11 alfajiri, mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka 18 amepatikana akiwa hai katika eneo lile lile alikodaiwa kuchukuliwa na mamba. Cha kushangaza zaidi ni kwamba alikutwa bila majeraha wala michubuko yoyote mwilini.
Kwa mujibu wa taarifa, wavuvi waliokuwa wakifanya shughuli zao kandokando ya Ziwa Victoria ndiyo waliomkuta binti huyo akiwa amelala karibu na ufukwe wa ziwa. Hata hivyo, hakuwa na uwezo wa kuzungumza. Wananchi kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi walimchukua na kumpeleka katika Hospitali ya Wilaya ya Ukerewe (Bomani) iliyopo Nansio kwa ajili ya matibabu na uchunguzi zaidi.
Akizungumza hospitalini hapo Machi 9, 2026, baba wa mwanafunzi huyo, Deonatus Salvatory, amesema familia ilishakata tamaa baada ya juhudi za kumtafuta kugonga mwamba. Alieleza kuwa walikuwa tayari wameanza maandalizi ya msiba na jamii ilikuwa imeanza taratibu za maombolezo kama ilivyo katika misiba mingine.
Salvatory amesema walipokea simu kutoka kwa wavuvi alfajiri wakitoa taarifa kuwa binti yao amepatikana kandokando ya ziwa akiwa hai, jambo lililowashangaza sana.
“Matumaini ya kumpata yalikuwa yamekwisha kabisa. Baada ya kutoonekana kwa muda mrefu tuliweka msiba na kufanya matanga, watu walikuwa tayari wameanza kutawanyika. Tangu nizaliwe katika eneo hili, sijawahi kushuhudia tukio kama hili. Tunaamini si jambo la kawaida,” amesema Salvatory.
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Ukerewe (Bomani), Dk. Bunhya Kayila, amesema walimpokea mwanafunzi huyo majira ya saa 1 asubuhi akiwa dhaifu. Uchunguzi wa awali umeonyesha hana majeraha yoyote yanayoashiria kuwa alishambuliwa na mamba.
Dk. Kayila amesema vipimo mbalimbali vinaendelea kufanywa ili kubaini hali yake kiafya, huku akieleza kuwa kwa sasa mwanafunzi huyo anaweza kutambua mazingira yanayomzunguka lakini bado hana uwezo wa kuzungumza. Amewekwa wodini chini ya uangalizi wa karibu kwa angalau saa 24.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe, Goodluck Mtigandi, amesema uchunguzi wa awali haujaonyesha dalili za uwepo wa mnyama hatarishi katika eneo alikodaiwa kushambuliwa mwanafunzi huyo.
Amesema tangu Machi 2 hadi sasa hakukuwa na ushahidi wowote wa kuthibitisha kuwa mnyama pori alimshambulia binadamu katika eneo hilo. Hivyo, mamlaka zinasubiri mwanafunzi huyo apate nafuu ili aweze kueleza kwa undani kilichotokea katika kipindi chote alichokuwa hajulikani alipo.
Aidha, Jeshi la Polisi Wilaya ya Ukerewe kupitia dawati la jinsia na watoto limezuia vyombo vya habari kumuona mwanafunzi huyo au kupiga picha zake. Kwa sasa amehamishwa wodini na anaendelea kuwa chini ya uangalizi wa karibu wa vyombo vya usalama pamoja na wataalamu wa afya huku uchunguzi zaidi ukiendelea kubaini ukweli wa tukio hilo.
Tupe maoni yako

0 comments:
Post a Comment