
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza, Amina Makilagi amesema kuwa hadi sasa hakuna tukio la kifo na upotevu wa mali ya mwananchi yeyote katika hekaheka za mvua kubwa iliyonyesha leo Machi 10, 2026 jijini Mwanza.
Mvua hiyo imenyesha mfululizo kwa takribani saa nane kuanzia saa 10 alfajiri hadi saa saba mchana na kuathiri maeneo mengi ya wilaya ya Nyamagana (jiji la Mwanza) hususan Kata ya Mkuyuni na kusababisha kubomoa kuta za majengo, magari kuzama, nyumba kuzingirwa na maji, na wananchi kushindwa kufanya shughuli ikiwamo kwenda kazini kutokana na maji kujaa barabarani.
Akizungumza leo na waandishi wa habari baada ya kutembelea eneo la Mkuyuni lililoathirika na mvua hizo, Amina amelipongeza jeshi la polisi na zimamoto kwa juhudi kubwa za kuhakikisha wananchi hawaathiriki na mvua hizo.
“Mpaka sasahivi ninavyozungumza hakuna mwananchi yeyote aliyepata tukio ama kifo chochote kilichotokea kwenye wilaya yetu, mtu aliyepoteza mali zake wala mtu yeyote kupata tatizo lolote la kiusalama, nashukuru jeshi la zimamoto wamefika kwa wakati na wameingia majini ndiyo maana utaona hata wale walioteleza wakaanguka kwenye maji waliokolewa,” amesema Amina.
Aliwataka wananchi kuwa makini na kuzingatia taarifa za utabiri wa hali ya hewa zinazotolewa kuhusu uwepo wa mvua kubwa, huku akiwataka wakazi wa mabondeni kuchukua hatua mapema kwa kutafuta maeneo yenye usalama.
Baadhi ya wakazi wa jiji la Mwanza, wakizungumzia hali hiyo walisema imewaathiri kwa kiasi kikubwa kwa kusababishwa washindwe kwenye kwenye maeneo yao ya kazi na kurudia njiani, kupoteza mali, biashara na kuhangaika kupata usafiri.
Abel Zabron, mkazi wa Nyegezi alisema changamoto hiyo ilimpata asubuhi wakati akielekea kazini ndipo alipofika Mkuyuni na kukuta maji yamejaa barabarani na kwenye makazi ya watu na kushindwa kuvuka kwenda upande wa pili (mjini).
Zabron alishauri serikali kuona namna ya kutengeneza miundombinu bora ikiwemo mito itakayokuwa inatiririsha maji vizuri ili barabara ziwe safi kwa ajili ya watu kuwahi makazini kwao.
Mkazi wa Butimba, Getrude Jacob alisema; “Hali ya leo imetuathiri sana tulikuwa na zana zetu lakini zote zimeondoka, hapa tulipo hatuan hata mbele wala nyuma nimeathirika sana na hii mvua na imeharibu vitu vingi sana. Nilikuwa natunzia vitu vyangu hapo garden lakini vimeenda vyote hapa nilipo sina mtaji yaani natetemeka tu,”
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment