ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Wednesday, March 25, 2026

AUA NA KUJERUHI KISA USHABIKI WA SIMBA NA YANGA

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa.


Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linamtafuta kijana mmoja (jina limehifadhiwa) kwa tuhuma za kumuua Abel Mganga Mazuri (25), mkazi wa Nyamahengo wilayani Kwimba, kwa kumchoma na kitu chenye ncha kali kifuani, pamoja na kuwajeruhi watu wawili.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Machi 25, 2026 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa, tukio hilo lilitokea Machi 24, 2026 majira ya saa 5:30 usiku katika kitongoji cha Nyamahengo, kata ya Sumve.

Inaelezwa kuwa mtuhumiwa alifanya shambulio hilo wakati akiwa na wenzake wakinywa pombe na kuangalia mpira katika banda la maonesho ya mpira, ambapo ugomvi ulizuka kutokana na ushabiki wa timu za Simba SC na Yanga SC.

Kamanda Mutafungwa amesema mtuhumiwa aliwashambulia watu watatu kwa kutumia kitu chenye ncha kali kufuatia mabishano makali yaliyochochewa na ushabiki huo, na kusababisha kifo cha Abel Mazuri.

Waliopata majeraha katika tukio hilo wametajwa kuwa ni Semen Juma Cherehani (26) na Ndubu Mkoi Chagula (26), ambao walijeruhiwa katika maeneo ya mikononi.

Jeshi la Polisi limeeleza kuwa majeruhi wote wamepatiwa fomu za matibabu (PF3) na wanaendelea kupatiwa huduma katika Hospitali Teule ya Sumve, huku hali zao zikiripotiwa kuimarika.

Aidha, Polisi wanaendelea na msako mkali wa kumkamata mtuhumiwa ili afikishwe katika vyombo vya sheria, huku wakitoa wito kwa wananchi kuepuka vurugu zinazotokana na ushabiki wa mpira uliopitiliza mipaka.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment