![]() |
| Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, SACP Jumanne Muliro (anayeongoza msafara) |
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, SACP Jumanne Muliro, amewataka askari wa Jeshi la Polisi kuacha mara moja kuingilia majukumu ya mamlaka nyingine, ikiwemo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kufuatia malalamiko ya wafanyabiashara wa Kariakoo kuhusu kunyanyaswa.
Akizungumza wakati wa ziara yake katika eneo la Kariakoo, Kamanda Murilo alikutana na wafanyabiashara wa Jumuiya ya Raha Square kwa lengo la kusikiliza na kutatua changamoto za kiusalama. Alisisitiza kuwa si jukumu la polisi kukagua mizigo ya wafanyabiashara wala kushughulikia masuala ya kodi, na kuonya kuwa askari watakaokiuka maelekezo hayo watachukuliwa hatua kali.
Awali, wafanyabiashara walilalamikia tabia ya baadhi ya askari kusimamisha mizigo yao katika makutano ya barabara na kukagua risiti za biashara, wakieleza kuwa hali hiyo imekuwa kero na chanzo cha usumbufu mkubwa.
Akizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara, Mwenyekiti wa Kijiwe cha Raha Square, Rweyemamu Erasto, alisema licha ya changamoto hiyo, pia wanakabiliwa na hali duni ya usalama hasa nyakati za usiku wanapofunga biashara zao. Alibainisha kuwa baadhi ya barabara bado hazijafunguliwa ipasavyo, hali inayochangia vitendo vya uporaji, huku biashara zinazofanyika barabarani zikiziba njia na kuongeza hatari ya ajali.
Aidha, wafanyabiashara walieleza wasiwasi wao kuhusu ongezeko la watoto wa mitaani wanaozagaa nyakati za usiku pamoja na uwepo wa watu wasiokuwa na utambulisho unaoeleweka, wakidai hali hiyo inahatarisha usalama wao na mali zao.
Katika mapendekezo yao, waliomba kufunguliwa kwa barabara zote za Kariakoo, kuondolewa kwa biashara zisizo rasmi barabarani, pamoja na kufungwa kwa mifumo ya kamera za ulinzi (CCTV) ili kusaidia kudhibiti uhalifu.
Akijibu hoja hizo, Kamanda Murilo amesema Jeshi la Polisi linaendelea kushirikiana na mamlaka mbalimbali kuhakikisha eneo la Kariakoo linakuwa salama. Aliahidi kufanyia kazi changamoto zote zilizotolewa na wafanyabiashara.
Kuhusu tatizo la watoto wa mitaani, alieleza kuwa Serikali kwa kushirikiana na taasisi husika inaendelea kutafuta suluhisho la kudumu kwa kuchunguza chanzo cha tatizo hilo. Pia alionya juu ya matumizi holela ya bajaji na maguta katika barabara kuu, akisema hatua madhubuti zitachukuliwa kudhibiti hali hiyo kwa kushirikiana na vyombo vya usalama.
Kamanda Murilo amesisitiza umuhimu wa matumizi ya teknolojia ya kamera za ulinzi, akibainisha kuwa zimekuwa msaada mkubwa katika kubaini na kudhibiti uhalifu.
Amemalizia kwa kuwahakikishia wafanyabiashara wa Kariakoo kuwa Jeshi la Polisi litaendelea kutoa ulinzi wa saa 24 ili kuhakikisha usalama wa watu na mali zao.
Tupe maoni yako

0 comments:
Post a Comment